*Kuwasaidia wahudumu wa afya kukabiliana na mitanziko ya kimaadili katika kufanya maamuzi ya ute ndaji wa matibabu

Na Mwandishi Wetu, Mbeya

Mtanziko wa kimaadili wakati wa kufanya maamuzi ya kutibu wagonjwa ni miongoni mwa changamoto inayowakumba watoa huduma za afya nchini wakati mwingine ikisababisha vifo kwa wagonjwa hasa pale wanapokataa matibabu.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Idara ya Falsafa na Taaluma za Dini kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Oslo nchini Norway kimezindua Kamati ya kwanza ya Maadili ya Kitabibu itakayowasaidia watoa huduma za afya katika kukabiliana na mitanziko(Dilemma) wanayokutana nayo wajkati wa kufanya maamuzi ya kutibu wagonjwa.

Kamati hiyo ambayo ni tofauti na kamati za maadili ya kiutumishi zilizozoeleka, inaundwa ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa miaka mitano unaofahamika kama ETHIMED.

Akizungumza mapema leo Februari 5, 2024 mara baada ya kuzindua kamati hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hosipital ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Dk. Godlove Mbwanji amesema kuwa kuundwa kwa kamati hiyo ni msaada mkubwa kwa watoa huduma za afya hasa wakati wakufanya maamuzi ya kutibu wagonjwa.

“Leo tumefungua mafunzo ya siku sita ambayo yatahusisha watumishi kwa maana ya watoa huduma za afya kutoka hospitali ya Rufaa ya Kanda-Mbeya ambao ndiyo wanaounda kamati ya maadili ya kitabibu ambayo itakuwa yakwanza kuanzishwa nchini, na hospitali yetu ndiyo yakwanza kuwa na kamati hii.

“Watoa huduma za afya wamekuwa wakikutana na mitanziko(Dilemma) hasa wakati wakufanya maamuzi yakutibu wagonjwa. Sasa mara nyingi wataalamu wakikutana na changamoto hizo kila mmoja anakuwa anahangaika kuwa afanye nini, sasa kuna masuala ya kimaadili kwamba nafanya maamuzi lakini je yanazingatia maadili ya kitatibu ili mwisho yasilete madhara kwa mgonjwa au kwa mtoa huduma.

“Hivyo, kamati hii imeundwa na itakuwa na mafunzo ya siku sita, tunaamini kuwa baada ya mafunzo haya kamati hii itaweza kufanya kazi nzuri yenye ufanisi katika kusaidia watoa huduma za afya.

“Hivyo sisi kuwa hospitali ya kwanza kuwa na kamati hii tunaamini tutasaidia hospitali nyingine nchini kujifunza namna ya kushughulikia mitanziko ya kimaadili kwa watoa huduma za afya na hatimaye kuboresha zaidi huduma kwa wagonjwa,” amesema
Dk. Mbwanji.
Lucas Kitula ni Mhadhiri msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Falsafa Taaluma za Dini na Mratibu wa mradi wa ETHIMED unaohusiana na maadili ya kitabibu kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Oslo nchini Norway akizungumzia kamati hiyo inayoundwa na watu 12 kutoka hospitali ya rufaa ya Kanda Mbeya amesema kuanzishwa kwa kamati hiyo ni mwanzo katika kuhakikisha kuwa elimu hiyo ya maadili ya kitabibu inazifikia hospitali nyingine nchini.

“Tunajua kuwa mitanziko hii ya kimaadili ipo sana kwenye hospitali zetu, hivyo kuanzisha kamati hii hapa Mbeya ni mwanzo kwani kama tutapata fedha huko mbele tutaweza kuzifikia hospitali nyingi zaidi, kwani hii ni muhimu sababu ni tofauti na kamati za maadili ya kiutumishi badala yake hii inawasaidia wahudumu wa afya kukabiliana na mitanziko wakati wa kufanya maamuzi ya utoaji huduma kwa wagonjwa.

“Mradi wetu wa ETHIMED ambao umeanza mwaka 2022 utakaoisha 2026 unalenga kuanzia hapa Mbeya na baada ya kamati hii tutakuwa tunafanya semina kwa ajili ya kufuatilia maendeleo kuona kama tuliyowafundisha wanayafanyia kazi kama inavyopaswa kuwa,” amesema Kitula.
Upande wake, Mkuu wa Idara ya Falsafa na Taaluma za Dini kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Michael Lyakulwa, amesema mradi huu utasaidia kutatua mitanziko mbalimbali ya kimaadili wakati wa kutoa matibabu kwa wagonjwa.

“Sisi kama idara na chuo kwa ujumla wajibu wetu ni kuhudumia jamii, hivyo mradi umetusaidia katika kuangalia ni kwa namna gani wataalamu wetu wa afya wanaweza kufanya maamuzi pindi wanapopata mitanziko wakati wa utoaji huduma.

“Hospitali ya rufaa ya kanda Mbeya ni ya kwanza kuwa na kamati hii ya maadili ya kitabibu, hivyo tunategemea kuwa Wizara ya Afya itatuunga mkono kuhakikisha kuwa kamati hizi zinaundwa katika hospitali zetu nchini ili kuwasaidia watoa huduma za afya wakati wapokumbana na mitanziko katika kufanya maamuzi ya utoaji huduma kwa wagonjwa,” amesema Dk. Lyakulwa.

Upande wake, Mhadhiri msaidizi Idara ya Falsafa na Taaluma za Dini kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu katika Maadili ya Kitabibu-Chuo Kikuu cha Oslo nchini Norway, Shija Kuhumba amesema mafunzo hayo yanalenga kuangalia namna kamati inavyopaswa kuwa pamoja na majukumu yake.

“Huu ni mwendelezo wa kile tulichofanya mwaka jana wa kutoa mafunzo ambapo sasa tumenzisha kamati ambayo kazi yake kuu itakuwa ni kutafakari mitanziko inayotokea katika kati utendaji kazi mfano; mgonjwa kukataa tiba, hii hali huwapa wakati mgumu watoa huduma za afya katika kufanya maamuzi ya kutibu wagonjwa. Hivyo, kwa kuwa na chombo hiki kutasaidia kutoa majibu ya changamoto ikiwamo ushauri,” amesema Kuhumba.

Mmoja wa wataalamu wa maadili ya kitabibu kutoka Chuo Kikuu cha Oslo nchini Norway, Dk. Berit Hofset Larsen ambaye pia ni Katibu wa kamati ya Maadili katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Norway, amesema kuundwa kwa kamati hiyo kutasaidia kuepusha mitanziko mingi ambayo imekuwa ikijitokeza wakati wa utoaji huduma za afya kwa watumishi.

“Tunafurahi kuona kwamba kamati hii imenzishwa hapa nchini nasisi jukumu letu nikusaidia kutoa mafunzo na uzoefu wetu ambao tumekuwa nao, hivyo tunaamini kuwa huu utaenda kuwa msaada kwa watoa huduma za afya hapa Tanzania,” amesema Dk. Larsen.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...