Na Mwandishi wetu Bungeni-Dodoma

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Mhe Dkt Festo Dugange amesema katika mwaka wa fedha 2024/25 Serikali kupitia mapato ya ndani, Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara itatenga Sh Milioni 70 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje katika Kituo cha Afya Likombe mkoani Mtwara.

Mhe Dkt Dugange ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe Tunza Malapo aliyehoji ni lini Serikali itakarabati jengo la ‘OPD’ na kujenga uzio katika kituo cha afya Likombe-Mtwara Mikindani.

Amesema Kituo cha Afya Likombe ni moja ya vituo vya afya vilivyonufaika na mpango wa maboresho ambapo katika mwaka wa fedha 2017/18 kituo hicho kilipokea Sh Milioni 500 na kujenga jengo la wazazi, maabara, jengo la kuhifadhia maiti, stoo ya dawa, nyumba ya mtumishi na kichomea taka.

“ Pamoja na maboresho makubwa yaliyofanywa katika kituo hicho bado kuna uhitaji wa jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje (OPD) pamoja na uzio.

Katika mwaka wa fedha 2024/25 Serikali kupitia mapato ya ndani, Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara itatenga Sh Milioni 70 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje katika Kituo cha Afya Likombe,” Amesema Mhe Dkt Dugange.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...