Na Seif Mangwangi,Arusha
WAZIRI wa nchi ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amewataka watendaji na maafisa wa ngazi za juu Serikali kuacha ubinafsi wa kutotambua na kuthamini (Appreciate), kazi zinazofanywa na wasaidizi wao jambo ambalo limekuwa likipunguza ufanisi Serikalini.
Simbachawene ameyasema hayo leo Februari 6, 2024 Jijini hapa alipokuwa akifungua mkutano wa 4 wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) unaoendelea katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha AICC Jijini Arusha.
Amesema tabia ya mabosi kutotambua kazi zinazofanywa na wasaidizi wao imekuwa ikipunguza ufanisi kazini na jambo hilo limekuwa likisababishwa na ufanisi mdogo wa mabosi hao ambao wamekuwa wakiogopa endapo watatambua kazi zinazofanywa na wasaidizi wao wanaweza kupoteza nafasi zao.
“Mimi ninachojua bosi anayejiamini hupaswa kutambua kazi inayofanywa na msaidizi wake ili kumfanya yeye bosi kuendelea kuaminika na kupata vyeo vikubwa zaidi, lakini kuna wengine wamekuwa wabinafsi kupindukia, hawataki kutambua kazi zinazofanywa na wasaidizi wao wakiogopa kupoteza nafasi, naombeni mbadilike,”amesema.
Amesema tabia ya ubinafsi imekuwa ikiwafanya baadhi ya watendaji wakuu serikalini kuendelea kubaki katika nafasi zao kwa muda mrefu pasipo kupandishwa vyeo huku wasaidizi wao wakihamishwa idara na kupanda vyeo baada ya kazi wanazofanya kuonekana.
Aidha Simbachawene ameupongeza uongozi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao chini ya Mkurugenzi wake Benedict Ndomba na kusema tangu Serikali ilipotunga sheria ya kuanzishwa kwa mamlaka hiyo, tayari kazi kubwa imefanywa na huduma nyingi zimeweza kuunganishwa mtandaoni.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Benedict Ndomba amesema kikao kazi hicho kimewakutanisha wadau wa Serikali Mtandao kutoka katika taasisi na mashirika mbalimbali ya umma, ili kujadili jitihada mbalimbali za utekelezaji wa Serikali Mtandao na kuweka mikakati itakayosaidia kukuza na kuimarisha Serikali Mtandao nchini.
Amesema katika kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan, Mamlaka ya Serikali Mtandao imefanikiwa kujenga mfumo unaowezesha mifumo ya TEHAMA ya Serikali kuwasiliana na kubadilishana taarifa, ujulikanao kama Government Enterprises Service Bus (GoVESB), ambapo tayari taasisi za umma 109 zimeunganishwa na mifumo 117 imesajiliwa.
Ndomba amesema washiriki katika kikao hicho ni zaidi ya wadau 1,000 wa Serikali Mtandao, kutoka katika taasisi na mashirika mbalimbali ya umma wakiwemo; Makatibu Wakuu, Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma, Makatibu Tawala Mikoa na Wilaya, Wakuu wa Vitengo na Idara za TEHAMA, Maafisa TEHAMA Pamoja na watumiaji wengine wa TEHAMA katika taasisi hizo kwa lengo la kujadili na kutoa taarifa ya hali ya utekelezaji wa jitihada za serikali mtandao katika taasisi za umma
Mamlaka ya Serikali Mtandao(e-GA), ni Taasisi ya Umma iliyoanzishwa kwa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019, ikiwa na majukumu ya kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao katika taasisi za umma, pamoja na kusimamia uzingatiaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa Taasisi za Umma.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Benedict Ndomba akitoa maelezo ya shughuli zinazofanywa na mamlaka hiyo kwa Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene alipotembelea banda la maonyesho la Mamlaka hiyo.
Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene akifungua Mkutano wa 4 wa kikao kazi cha Mamlaka ya Serikali Mtandao unaoendelea Jijini Arusha (Picha zote na Seif Mangwangi)
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala bora George Simbachawene akiwasili kwenye viwanja vya ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa AICC kabla ya kuanza kutembelea mabanda ya maonyesho ya kazi za taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi kuhusu Serikali Mtandao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...