KAMPUNI Ya Swissport Tanzania imesaini makubaliano ya miaka mitatu na Taasisi ya CCBRT ambapo Swissport Tanzania itatoa shilingi milioni 40 kwa miaka mitatu kwa Taasisi hiyo kwa ajili ya matibabu ya miguu vifundo kwa watoto waliozaliwa na changamoto hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Swissport Tanzania Mrisho Yassin amesema, wamejenga mahusiano mazuri na CCBRT na kuvutiwa na namna huduma zinavyotolewa hususani kwa wenye matatizo ya viungo na kuamua kuunga mkono jitihada hizo za utoaji huduma kwa wananchi.
Mrisho amesema kuwa, kwa mujibu wa makubaliano hayo kwa miaka mitatu watatoa milioni 40 kila mwaka kwa ajili ya kusaidia matibabu ya urekebishaji wa watoto waliozaliwa na miguu vifundo.
Aidha ameipongeza CCBRT kwa jitihada kubwa wanayoifanya katika kusaidia jamii na kuahidi kuendelea kushirikiana nao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya CCBRT Brenda Msangi amesema; makubaliano hayo ya miaka mitatu yanawapa ujasiri wa kutoa huduma.
"Kila mwaka kwa miaka mitatu tutakuwa tunapokea shilingi milioni arobaini kutoka Swissport Tanzania ambapo watoto hamsini wenye tatizo la mguu kifundo au waliozaliwa na mguu kifundo tunaenda kubadilishana maisha yao." Ameeleza Brenda.
Amesema, kuna watoto ambao hawapati matibabu hayo na kuendelea kupata ulemavu wa kudumu ambao ungeweza kurekebishika na watoto hao kwenda shule, kufanya kazi na kuwa na mchango katika jamii na lengo CCBRT ni kuhakikisha watoto wenye tatizo hilo hawapati ulemavu wa kudumu kwa kuwa tatizo la mguu kifundo linarekebishika.
Pia amesema CCBRT inahitaji wadau mbalimbali wa kuwashika mkono katika kufanikisha dhima ya Taasisi hiyo ya kuamua kuwasaidia watu wanaotoka mazingira magumu na kuishukuru Swissport Tanzania kwa kuwashika mkono katika kubadilisha maisha ya watanzania.
Aidha ameishukuru Swissport Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo ambapo awali walitoa mashine ya Ultrasound ambayo hadi sasa imesaidia watanzania wengi.
Kwa mujibu wa Brenda watoto wapatao 2400 huzaliwa na tatizo la mguu kifundo kila mwaka na matibabu ya kurekebisha tatizo hilo hufanyika kwa miaka mitano ambapo changamoto za gharama husababisha baadhi ya wazazi kutokamilisha mfululizo wa urekebishaji wa tatizo hilo hali inayopelekea watoto kurudi kwenye hali ya awali inayopelekea ulemavu wa kudumu.
Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya CCBRT Brenda Msangi (Kulia,) na Mkurugenzi Mtendaji wa Swissport Tanzania Mrisho Yassin (Kushoto,) wakisaini hati za makubaliano hayo ya miaka mitatu ambapo Swissport Tanzania itagharamia matibabu ya marekebisho kwa watoto wenye miguu vifundo. Leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya CCBRT Brenda Msangi (Kulia,) na Mkurugenzi Mtendaji wa Swissport Tanzania Mrisho Yassin (Kushoto,) wakionesha hati za makubaliano hayo.
Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya CCBRT Brenda Msangi akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano hayo na kutoa rai kwa watanzania na kampuni mbalimbali kusaidia matibabu ya miguu vifundo kwa watoto ambayo yanarekebishika na kuondoa ulemavu wa kudumu. Leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Swissport Tanzania Mrisho Yassin akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano hayo na kueleza kuwa kampuni hiyo itaendelea kushiriki katika kusaidia jamii kwa mujibu wa sera ya kampuni hiyo. Leo jijini Dar es Salaam.


Matukio mbalimbali wakati wa hafla hiyo iliyofanyika katika Taasisi ya CCBRT jijini Dar es Salaam.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...