TANZANIA imeweka alama kubwa ya mafanikio katika maendeleo na ustawi wa sekta ya masoko ya mitaji katika kipindi cha mwaka 2023, ambapo bidhaa mpya na bunifu zinazowezesha kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi zimeidhinishwa na kuorodheshwa katika soko la hisa kwa mafanikio makubwa.

Hayo yameelezwa leo Februari 13, 2024 jiijini Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana CPA.Nicodemus Mkama wakati wa hafla ya wadau wa masoko na mitaji kuhusu tathimini ya mwenendo wa masoko ya mitaji kwa mwaka 2023.

Akitaja bidhaa hizo ambazo zimeidhinishwa ni pamoja na hatifungani za kijani yaani green bond, hatifungani zenye mguso kwa jamii yaani social bond na hatifungani zenye kukidhi misingi ya Shariah yaani Sukuk bond.

Amesema matokeo hayo yameiweka Tanzania katika ramani ya masoko ya mitaji ulimwenguni yanayotoa bidhaa mpya na bunifu, zinazovutia wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.

"Mafanikio hayo yametokana na mazingira wezeshi, shirikishi na endelevu ya kisera, kisheria na kiutendaji ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi madhubuti wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, " amesema.

Aidha, amesema sera za uchumi wa kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa zinazotekelezwa chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, zimekuwa chachu yenye matokeo chanya katika kukuza ushiriki wa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa na hivyo kuleta mafanikio makubwa zaidi katika masoko ya mitaji.

Amefafanua CMSA, ambayo ni Mamlaka yenye jukumu la kusimamia na kuendeleza masoko ya mitaji hapa nchini imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza mikakati ambayo imewezesha kufikia mafanikio hayo.

Amesema mamlaka imetekeleza mikakati ambayo imewezesha kufungua Nyanja na fursa mpya katika masoko ya mitaji.Ametaja mikakati hiyo ni kuanzisha bidhaa na huduma mpya, bunifu, zenye mlengo maalum na matokeo chanya kwa jamii.

Mikakati mingine ni matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika kutoa huduma; kuongeza idadi ya wataalamu wanaokidhi viwango vya kimataifa; na kutoa elemu kwa umma kuhusu fursa zinazopatikana katika masoko ya mitaji.

Ameongeza kuwa jitihada hizo zimechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji na mauzo katika soko la hisa, ambapo thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji imeongezeka kwa asilimia 10.1 na kufikia Sh. trilioni 37.4 katika kipindi kilichoishia Desemba 2023, ikilinganishwa na shilingi trilioni 33.9 katika kipindi kilichoishia Desemba 2022.

"Jumla ya mauzo ya hisa na hatifungani yameongezeka kwa asilimia 31.0 na kufikia shilingi trilioni 4.2 katika kipindi kilichoishia Desemba 2023, ikilinganishwa na Sh. trilioni 3.7 katika kipindi kilichoishia Desemba 2022.

"Mauzo ya hatifungani yameongezeka kwa asilimia 29.4 na kufikia Sh. trilioni 3.9 katika kipindi kilichoishia Desemba 2023, ikilinganishwa na Sh. trilioni 3.0 katika kipindi kilichoishia Desemba 2022...

" Na Mauzo ya hisa yameongezeka kwa asilimia 68.5 na kufikia shilingi bilioni 225.2 katika kipindi kilichoishia Desemba 2023, ikilinganishwa na shilingi bilioni 133.7 katika kipindi kilichoishia Desemba 2022.

Aidha, thamani ya mifuko ya uwekezaji wa pamoja imeongezeka kwa asilimia 51.2 na kufikia shilingi trilioni 1.8 katika kipindi kilichoishia Desemba 2023, ikilinganishwa na shilingi trilioni 1.2 katika kipindi kilichoishia Desemba 2022.

CPA.Mkama amesema pia fungu la 10 la Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana limeipa CMSA jukumu la kuanzisha kuendeleza na kusimamia masoko ya mitaji hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kuandaa kanuni na miongozo ya utoaji wa bidhaa na huduma mpya, bunifu na zenye mlengo maalum.

Hivyo katika kutekeleza jukumu hilo katika kipindi cha mwaka 2023, CMSA imeshirikiana na wadau wa masoko ya mitaji kuandaa miongozo ya kuendesha na kusimamia bidhaa za mitaji halaiki.

Amefafanua bidhaa hizo zitawezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo za kampuni changa, ndogo na za kati.

Aidha, CMSA imeshirikiana na wadau wa masoko ya mitaji kuandaa miongozo ya utoaji wa hatifungani zinazokidhi misingi ya Shariah yaani Guidelines for Corporate Sukuk Bonds. Miongozo hiyo imeidhinishwa na Wizara ya Fedha na imefanikiwa kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali kwa matumizi ya umma.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana CPA.Nicodemus Mkama akigpnga kengele kuashiria bidhaa mpya na bunifu zinazowezesha kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi zimeidhinishwa na kuorodheshwa katika soko la hisa (DSE) kwa mafanikio makubwa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana CPA.Nicodemus Mkama akizungumza jambo mbele ya wageni waalikwa mbalimbali wakati wa hafla ya wadau wa masoko na mitaji iliyohusu tathimini ya mwenendo wa masoko ya mitaji kwa mwaka 2023.















Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...