CapeTown

Balozi wa Tanzania Jamhuri ya Afrika Kusini Mhe. James Bwana amesema Tanzania inayo mengi ya kujifunza kwenye Mkutano wa Uwekezaji wa Madini Barani Afrika wa Mining Indaba utakaofanyika kuanzia tarehe 5 hadi 8 Februari, 2024 nchini Afrika Kusini.

Mbali ya kuwa Balozi wa Afrika Kusini pia, Mhe. balozi Bwana anaiwakilisha Tanzania katika nchi za Jamhuri ya Botswana na Ufalme wa Lesotho.

Ameyabainisha hayo leo Februari 4, 2024 wakati akizungumza katika mahojiano maalum baada ya kuzungumza na Ujumbe wa Tanzania unaotarajia kushiriki katika Mkutano huo utakaofanyika katika Hotel ya Westin ambapo mwaka huu unatimiza miaka 30 tangu kuanza kwake.

Amesema Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zenye utajiri mkubwa wa madini Afrika na duniani inatarajia kunufaika vilivyo kupitia mkutano huo na hususan kujifunza mengi kutoka katika nchi ya Afrika Kusini ambayo imepiga hatua kubwa katika masuala mbalimbali kwenye mnyororo wa shughuli za madini ikiwemo yanayohusu uwekezaji kwenye sekta ya madini, teknolojia shughuli za uongezaji thamani madini pamoja na namna nchi hiyo inavyosimamia sekta ya madini.

Aidha, ameongeza kwamba, mbali na kujifunza kutoka katika nchi ya Afrika Kusini na mataifa mengine, pia Tanzania inatarajia kuutumia mkutano huo kunadi fursa zake za uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini.

'' Wenzetu katika Jamhuri ya Afrika Kusini wamepiga hatua kubwa katika sekta ya madini kwa hiyo kama nchi tunayo mengi ya kujifunza kutoka kwao na kutoka kwa nchi nyingine zinazoshiriki mkutano huo. Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi duniani ambazo zinafanya vizuri katika Sekta ya Madini na Rasilimali Madini imechangia kuwafikisha hapa," amesema balozi Bwana.

Wakati mkutano huo unatarajia kufunguliwa rasmi kesho Februari 5, 2024, leo Mawaziri kutoka nchi mbalimbali za Afrika wanaosimamia masuala yanayohusu madini wanakutana katika Kongamano kujadili mambo mbalimbali yanayohusu Sekta ya Madini Barani Afrika.

Kwa upande wa Tanzania, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa anaongoza ujumbe wa Tanzania katika kongamano hilo, akiambatana na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali, Balozi wa Tanzania nchini humo Mhe. Bwana, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Msafiri Mbibo, Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman Mwanga na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST). Dkt. Mussa Budeba.

Tanzania inashiriki kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Uwekezaji wa Mining Indaba kwa kushirikiana na Sekta binafsi inayowakilishwa na Chemba ya Migodi Tanzania ambapo kampuni mbalimbali zilizo chini ya mwanvuli huo zinashiriki.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...