Na Jane Edward, Arusha
Mtandao wa utetezi wa haki za watoto,wanawake na wasichana nchini (TAPO)umelaani vikali tukio la kupigwa na kuuawa kwa msichana wa jamii ya Kifugaji akiwa na ujauzito ,Nanyoli Mohee baada ya kugoma kuolewa bila idhini yake.
Neema Laizer ni moja kati ya viongozi wa mtandao huo anasema tukio hilo la kinyama limetokea mwanzoni mwa wiki hii katika kijiji cha Malambo wilayani Ngorongoro mkoa wa Arusha.
Anasema mwanaume wa jamii ya kifugaji kabila la wamaasai anayejulijana kwa jina la Amyor Matayo alimshambulia msichana huyo mwenye umri chini ya miaka 18 kwa kumpiga na fimbo mbele ya baba yake mzazi akimlazimisha kumpeleka nyumbani kwake kama mke kwa kuwa alishamlipia mahari kwa wazazi wake wakati akiwa bado tumboni kulingana na mila na desturi za jamii hiyo.
"Unajua jamii ya kimasai wakati mwingine mila na desturi zinakatisha utu wa mtu kwa mfano kutolewa mahari kwa mtoto akiwa tumboni hiyo unaona haijakaa sawa na inashusha utu wa mtu"Alisema
Awali binti huyo alichukuliwa na mwanaume huyo kwa ajili ya maisha ya ndoa lakini alitoroka nyumbani kwa mwanaume huyo na kwenda kuishi porini, lakini alikuja kugunduliwa na mpita njia ambaye aliamua kumrejesha nyumbani kwa wazazi wake.
Kwa mujibu wa mpita njia huyo anasema baba mtu alimpigia simu mume wa Binti huyo na alipofika alianza kuchapwa ambapo binti huyo alipiga kelele kutokana na maumivu aliyokuwa akiyapata na majirani walifika nyumbani kwa baba yake na kumkuta akiwa na hali mbaya na kuamua kumpeleka katika hospitali ya Malambo kwa ajili ya matibabu lakini siku iliyofuata alifariki dunia.
Naye Iddy Ninga kutoka Mtandao wa kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto alisema wao kama TAPO wamesikitishwa na tukio hilo na kutoa tamko kuwa mwili wa marehemu usizikwe hadi hapo uchunguzi wa kina utakapofanyika na taarifa ya uchunguzi ikabidhiwe kwa vyombo husika vya kisheria.
Pia wamevitaka vyombo vya ulinzi na usalama yakiwemo madawati ya kijinsia kutekeleza majukumu yake kikamilifu ili kuhakikisha haki inatendeka katika kushughulikia suala hilo na serikali .
Aidha wameutaka serikali ipeleke mswada kwa ajili ya mabadiliko ya kifungu cha 13 na 17 cha sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inayoruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 14.
Naye Rose Njilo Mkurugenzi wa Shirika la Mimutie women organization linalojihusisha na utetezi wa haki ya mtoto na wanawake katika jamii za pembezoni alisema matukio ya mabinti wenye umri mdogo kulazimishwa kuolewa yamekithiri kiasi kwamba yamekuwa yakisababisha vifo.
Alisisitiza kuwa ili kupunguza matukio hayo serikali kupitia wizara ya katiba na sheria inapaswa kuangalia sheria zake kwakuwa zime mruhusu msichana kuolewa akiwa na miaka kumi na tano na Mwanaume kuruhusiwa kuoa akiwa na miaka 18 kitu ambacho sio kizuri.
Alisema tukio jingine lilitokea katika kijiji cha Lufubu Mkoani Kigoma ambapo binti aliyefahamika kwa jina la Mbaru Juakali (17)alifariki dunia kwa kipigo cha baba yake mkùbwa baada ya kukataa kuolewa wakati wazazi wake wamepokea mahari ya ng'ombe 13.
TAPO wamedai kwamba watu wawili wanashikiliwa na jeshi la polisi wilayani humo ambao ni Mume wa marehemu pamoja na baba mzazi wa marehemu.
TAPO wakilaani kitendo cha kuuawa binti aliyekataa kulazimishwa kuolewa mbele ya vyombo vya habari.Neema Laiza akifafanua jambo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...