* JICA Yazidi kuleta neema kwa wanafunzi

VIJANA Nchini wameshauriwa kutumia fursa za Maendeleo ya teknolojia duniani kutatua changamoto katika jamii kwa kuzingatia mila na tamaduni za Tanzania.

Hayo yameeelezwa leo jijini Dar es Salaam na Balozi wa Japan nchini Yasushi Misawa wakati wa hafla ya kutafuta wazo bora la ubunifu na biashara (JICA Chair 2023,) kwa wanafunzi wa UDSM iliyofanyika chuoni hapo.

Amesema, Serikali ya Japan kupitia JICA itaendelea kushirikiana na Tanzania na taasisi za Elimu katika kusaidia vijana wenye mawazo bunifu ya kibiashara ili kunufaisha Taifa katika uchumi.

Balozi Yasushi amesema, uwepo wa makabila takribani 130 nchini ni fursa kwa vijana kutumia TEHAMA katika kutatua changamoto zinazowakabili kwa kuzingatia mila na tamaduni.

"Japan tumekuwa tukitumia mitindo ya kale na sasa katika kuboresha sekta za maendeleo, ni fursa kwa vijana na Tanzania kuendeleza biashara kwa mtindo wa Tanzania na kutanuka katika nchi nyingine." Amesema.

Aidha amesema kuwa uhusiano imara wa mataifa hayo mawili utaendelea kudumishwa na kuzidi kuzalisha bunifu nyingi na za kipekee.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkuu wa JICA Tanzania Ara Hitoshi amesema wamekuwa wakishirikiana na UDSM katika kukuza biashara na ubunifu kwa kuwalenga vijana na wanawake kupitia programu za JICA Chair kwa wanafunzi wa UDSM na Ninja Mwanamke mahususi kwa wanawake na wanaamini hiyo ni hatua kubwa ya kuwezesha vijana kupitia mawazo yao bunifu.

Pia Makamu Mkuu wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam anayeshughulikia Taaluma Prof. Nelson Boniphace amesema, chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM,) kinalea wanafunzi kibiashara kwa kushirikiana na Ubalozi wa Japan, JICA pamoja na Deloitte.

"Leo tumekuwa na uwasilishaji wabunifu makundi mbalimbali wakiwemo akina Mama kupitia programu ya Mwanamke Ninja ambao kupitia mawazo yao ya ubunifu tayari wameanza kuzalisha bidhaa mbalimbali ambazo ni bidhaa asilia za nywele ambazo mbunifu wa bidhaa hizo aliwahi kupata athari za kiafya kutokana na kutumia kemikali katika nywele pamoja na mbunifu wa programu ya Mipango App mahususi kwa vijana na wanawake katika kusimamia mapato, matumizi na kuweka akiba." Amesema.

Prof. Nelson amesema, changamoto kubwa inayowakabili wabunifu hao ni uzalishaji finyu ukilinganisha na idadi ya wateja.

Kuhusiana na wanafunzi waliopo chuoni hapo amesema kuwa; UDSM imekuwa ikiendeleza mawazo ya wanafunzi kibiashara kwa kutumia changamoto kama fursa zitakazoleta matokeo chanya kwa jamii ikiwemo katika sekta za afya na mazingira.

"Licha ya kutoa degree mbalimbali Chuo kikuu cha Dar es Salaam kinafanya kazi tatu ikiwemo kufanya tafiti, kutoa huduma kwa jamii pamoja na kufanya na kuendeleza bunifu kwa kuwasikiliza na kuwapa miongozo wanafunzi wenye mawazo bunifu ya kibiashara pamoja na kuwakutanisha na watu mbalimbali wanaoweza kushiriki katika kufanikisha mawazo yao na hiyo ni kupitia Kurugenzi ya Ubunifu na Ujasiriamali ya Chuo kikuu cha Dar es Salaam." Amesema.

Aidha ameishukuru Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA,) na Deloitte kwa kuendelea kukuza mawazo ya vijana kibiashara jambo litakalopunguza changamoto ya ajira pamoja bunifu hizo kuingia katika soko la Kimataifa.

Lilian Makoi mwanzilishi mweza wa Mipango App na mshindi wa Program ya Ninja Mwanamke amesema programu hiyo imewasaidia katika kuwajengea uwezo pamoja na kuboresha bidhaa ikiwemo katika kuingia ubia na kampuni nyingine na kutafuta wateja wapya.

Amesema, JICA kwa kushirikiana na Deloitte wamekuwa kinara kwa kuisaidia Mipango App kufikia walengwa wengi zaidi ambao ni wanawake na vijana na kuwawezesha kupata maarifa mapana ya elimu ya fedha na kuweka akiba.

Katika uwasilishaji wa mawazo bunifu kwa wanafunzi ( JICA Chair 2023,) Hyalosustainer. co. Ltd wameibuka kinara kupitia wazo la utengenezaji wa kemikali ya Hyaluronic Acid ambayo watumiaji huagiza nje ya nchi kwa ajili ya matumizi ya viwanda ikiwemo vya dawa, vipodozi na vifaa vya hospitali, huku nafasi za pili na tatu zikishikwa na mawazo bunifu ya utunzaji wa mazingira na Elimu ya afya ya uzazi.
 

Balozi wa Japan nchini Yasushi Misawa akizungumza wakati hafla uwasilishaji wa mawazo bunifu kwa wanafunzi wa UDSM kupitia programu ya JICA Chair 2023 na programu ya Ninja Mwanamke mahususi kwa wanawake na kuwashauri vijana kutumia TEHAMA katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi. Leo jijini Dar es Salaam.
 

Mwakilishi Mkuu wa JICA Tanzania Ara Hitoshi akizungumza wakati wa hafla ya na kueleza kuwa wataendeleza ushirikiano huo wenye tija ili kuinua vijana na wanawake wengi zaidi. Leo jijini Dar es Salaam.
 

Makamu Mkuu wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM,) anayeshughulikia Taaluma Prof. Nelson Boniphace akizungumza wakati wa hafla hiyo na kueleza kuwa licha ya kutoa shahada mbalimbali chuo hicho kinalea wanafunzi kibiashara. Leo jijini Dar es Salaam.



 

Matukio mbalimbali wakati wa hafla hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...