Na WAF - Dodoma

Wasajili wa Mabaraza ya Wataalamu na Bodi za Ushauri nchini wametakiwa kuweka mikakati na mifumo yenye tija itakayohakikisha wanataaluma wanazingatia weledi na Miiko ya taaluma zao ili kuongeza ubunifu katika utendaji na kuhakikisha watanzania wanapata hubuma bora za Afya nchini.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu Februari 22, 2024 jijini Dodoma katika kikao na Wasajili wa Mabaraza ya wataalam na Bodi ya Washauri kilichokua na lengo la kujadili namna ya kuzidi kuboresha huduma kwa wananchi.

Dkt. Jingu amewataka wasajili hao kuweka mifumo mahali pa kutolea huduma itakayowezesha kuibua upotovu wa Maadili au ukosefu wa weledi kwa wanataaluma kwa wakati hasa kwa kuwashirikisha viongozi wa ngazi za Mikoa.

Aidha, Dkt. Jingu amewataka wasajili hao kubaini na kuzizuia Changamoto za Maadili na weledi kabla hazijaleta madhara makubwa na wasibaki kuwa kama mahakimu wa kusubiri hadi matatizo yatokee ndio wachukue hatua.

“Gatueni majukumu yenu huko katika Mikoa na Halmashauri kwa kuzingatia sheria zilizounda Mabaraza yenu lakini kufanya hivyo hakuwaondolei majukumu yenu, bado mna jukumu la msingi la kusimamia weledi na Maadili ya wanataaluma katika Sekta yetu ya Afya". Amesema Dkt. Jingu.

Ameongeza kuwa Wananchi wanastahili kupata huduma bora hivyo wasajili wanapaswa kufuatilia na kufanyia kazi kero za wananchi ikiwa ni pamoja na malalamiko ili.kuongeza tija na ufanisi wa utendaji.

Dkt. Jingu ameelekeza mabaraza kujitangaza ili majukumu yake yajulikane na kuwawekea wananchi namna nzuri ili waweze kufika katika mabaraza kwa urahisi ili kutoa taarifa".

“Twendeni tukawajulishe wananchi kuwa sisi ni akina nani, majukumu yetu ni yapi na njia na mawasiliano zinazotumika ili kutufikia”. Amesema.

Mwisho, Dkt. Jingu amewataka wasajili hao kuacha kufanya kazi kwa nyezo za kizamani bali wazingatie na kutekeleza majukumu kwa kutumia teknolojia za kisasa za mawasiliano ili kuongeza uwajibikaji.

Awali akimkaribisha Katibu Mkuu kwenye kikao hicho, Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amesema ofisi ya Mganga Mkuu wa Serikali chini ya Wizara ya Afya ina jukumu la kusimamia Mabaraza nane ya kitaaluma ambapo miongoni mwa jukumu ni kusimamia weledi na maadili ya wataalamu pamoja na Bodi mbili za Washauri ambazo ni Bodi ya Maabara Binafsi (PHLB) na Bodi ya Ushauri wa Hospitali Binafsi (PHAB) zenye jukumu la kumshauri Waziri juu ubora wa huduma na kusajili maabara na hospitali binafsi.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...