Na Seif Mangwangi Mbarali


KUNDI kubwa la zaidi ya Ng'ombe 500 na punda3 wamekamatwa na askari wa Jeshi Usu la  Uhifadhi katika hifadhi ya Taifa  Ruaha Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya huku wamiliki wa mifugo hiyo wakikimbia .

Kwa mujibu wa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, shirika la hifadhi za Taifa Tanzania na Mkuu wa hifadhi ya Ruaha, Goodwill Meng'ataki amesema mifugo hiyo imekamatwa katika eneo la ukwaheri ndani ya bonde Oevu la Ihefu.

Akizungumza katika eneo ambalo mifugo hiyo imehifadhiwa baada ya kukamatwa, Meng'ataki amesema eneo hilo ambalo mifugo hiyo imekamatwa ni  katikati ya hifadhi ya Ruaha katika bonde la Ihefu mahala ambapo ni chanzo cha maji ya mto Ruaha mkuu.

Amesema baada ya kukamatwa kwa mifugo hiyo, walifikisha suala hilo Polisi na baadae katika Mahakama ya Wilaya ya Mbarali na tayari Mahakama imeshatoa hukumu ya kutaifishwa kwa mifugo hiyo nakuagiza iuzwe.

"Kwa kawaida tunavyokamata mifugo ndani ya hifadhi, tunawasiliana na Polisi na kuifikisha Mahakamani. Tayari Mahakama imetolea maamuzi mifugo iliyokamatwa na imeagiza iuzwe, tunasubiri wanunuzi ambao tayari wako njiani kuja hapa Ukwaheri kwaajili ya kununua,"amesema.

Amesema wafugaji katika bonde la Ihefu katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha,  wamekuwa wabishi kuelewa katazo la kutochungia mifugo yao ndani ya hifadhi hiyo na wamekuwa wakitumia mwanya wa eneo hilo kuwa na maji mengi kuingiza mifugo kwenye maeneo ambayo ni vigumu kufikiwa na Askari wa Jeshi Usu la Uhifadhi.

" Kipindi hiki Kuna mvua nyingi zinanyesha ukanda huu, hawa wafugaji wamekuwa wakitumia mwanya huo huo kuingiza mifugo yao kwenye maeneo yenye maji mengi wakijua Askari wetu hawawezi kufika huko, lakini tunajitahidi kukabiliana nao,"amesema.

Amesema changamoto nyingine ni Askari wake kukabiliana na wafugaji ambao wamekuwa wakitumia silaha za jadi ikiwemo mishale na mikuki pindi wanapokamatiwa mifugo yao wakitaka kuitorosha.

Afisa Uhifadhi daraja la pili na Mkuu wa Kanda ya Usangu, Abisai  Nassari amesema baada ya kukamata mifugo hiyo 547 na punda 3,  walitumia msaada wa helkopta kuisogeza  hadi katika eneo lenye maji machache ndipo askari wake wakaisogeza hadi eneo la ukwaheri.

"Tunashukuru Serikali ya Rais Mama Samia kutuletea vifaa vichache vinavyotusaidia kupambana na mifugo na majangili wa wanyamapori, tunaomba kuongezewa  vifaa zaidi ili tuweze kufanyakazi yetu kwa ufanisi zaidi,"anasema.

Anasema changamoto kubwa wanayokabiliwa nayo ni namna ya kuwakabili wafugaji wanaoingiza mifugo katika bonde la Ihefu kwa kuwa eneo hilo ni chepechepe lililojaa matope kutokana na kuteremsha maji wakati wote.

Licha ya kundi kubwa kukamatwa na kutaifishwa, mwandishi wa habari hizi akiwa ndani ya Helkopta angani bado aliweza kushuhudia baadhi ya makundi makubwa ya ng'ombe wakiwa ndani ya eneo Oevu la Ihefu katika hifadhi ya Ruaha.


 


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...