Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kukuza uchumi wa Sekta binafsi inayochangia makusanyo ya kodi ambazo zitawezesha ujenzi wa miundombinu ya barabara na utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo nchini.

Bashungwa amezungumza hayo Machi 27, 2024 katika kikao kilichowakutanisha wafanyabiashara wa Wilaya ya Karagwe pamoja na Taasisi za Serikali zinazowahudumia ambapo amesikiliza kero zao ikiwemo tozo kubwa za kodi, ushuru pamoja na kauli zisizoridhisha kutoka kwa Maafisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA).

Bashungwa amesisitiza kuwa ukusanyaji wa mapato unawezesha Serikali kufanikisha malengo yake ya kuhudumia nchi pamoja na wananchi wake kwa haraka kwa kuwa wajibu wa Serikali ni kujenga ustawi wa wafanyabiashara na sio kuwadumaza.

“Sijafurahishwa na madai ya kauli za Maafisa kwa wafanyabiashara ambazo sio sahihi,kwa kuwaaambia wakishindwa kulipa kodi, wafunge baishara, Lengo la Serikali ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwawezesha kwa kutoa elimu, kuwashauri na kustawisha wafanyabiashara” amesisitiza Bashungwa.

Aidha, Bashungwa ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa wa Kagera kusimamia miongozo pamoja na kutoa elimu ya Sheria na Kanuni za kodi mara kwa mara kwa wafanyabiashara pamoja na Maafisa kuwa na kauli nzuri na wezeshi.

Bashungwa amelitaka Baraza la wafanyabiashara la Wilaya ya Karagwe kutimiza wajibu wao kwa kuitisha mikutano ya mara kwa mara na wafanyabiashara wote ili kukumbushana masuala tozo mbalimbali zilizopo na kutatua changamoto zao kwa kuzipatia suluhu ya haraka kabla mfanyabiashara hajafikia hatua ya kufunga biashara.

Kuhusu utekelezaji wa miundombinu, Bashungwa amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa barabara ya Bugene-Benaco (km 128.5) pamoja na kuanza utekelezaji wa barabara ya Omurushaka - Kyerwa (km 50) na Omugakorongo – Kigarama - Murongo (Km 111) kwa kiwango cha lami.

Naye, Mfanyabiasha wa Kampuni ya SANOA, Bw. Metisela Philipo, ameeleza kuwa kodi na faini wanazotozwa zimekuwa kubwa na haziendani na biashara wanazozifanya hivyo kupelekea baadhi ya wafanyabiashara kufunga biashara zao.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Kagera, Bw. Omary Kigoda amesema kuwa suala la lugha mbaya kwa walipa kodi sio msimamo wa Taasisi hivyo TRA itaendelea kuwachukulia hatua baadhi ya watumishi ambao wanaenda kinyume na maadili ya utumishi.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Karagwe, Paschal Rwamugata amesema kuwa moja ya majukumu ya Chama ni kusikiliza kero za wananchi na kuitaka Serikali kutatua kero hizo kama ambavyo imekuwa ikifanya.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...