Na Mwandishi wetu Tanga

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeiagiza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupanga bajeti ya kutosha ili kuhakikisha majengo mapya ya maabara yanajengwa na yale yanayofanyiwa ukarabati yafanyiwe kwa ukamilifu.

Mwenyekiti wa Kamati Mhe Deudatus Mwanyika pamoja na Waheshimiwa wajumbe wa Kamati hiyo walitoa maagizo hayo wakati Kamati ikipokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya Ukarabati wa Maabara Kuu ya Udongo Kituo cha TARI Mlingano leo tarehe 15 Machi, 2024 jijini Tanga.

Taasisi hiyo iliomba jumla ya Shilingi 500,000,000/= Katika mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya ukarabati wa maabara ya udongo. Sambamba na ukarabati huo Kamati pia ilikagua ujenzi wa jengo jipya ambalo linahusika na Teknolojia ya namna ya uzalishaji miche kwa njia ya maabara (Tissue culture) ambapo mche mama mmoja unazalisha miche 20.

Kamati pamoja na wajumbe wamepongeza ukarabati huo uliofanyika, pamoja na kujionea vifaa vya maabara ambavyo ni vipya tayari kwa matumizi na kuendelea kusisitiza ukamilishwaji wa haraka ili maabara hizo ziweze kutumika.

Kwa upande wa TARI, walieleza changamoto zao kwa Mhe. Mwenyekiti pamoja na Waheshimiwa wajumbe kuwa Taasisi hiyo inapambana na uchakavu na uhaba wa vifaa na miundo mbinu, upungufu wa watumishi, uhaba wa maji na umeme usio wa uhakika pamoja na Maabara kutokuwa na ithibati (Accreditation) hivyo inawapasa kupeleka sampuli za udongo nje ya nchi.

Aidha, Kamati imeendelea kupongeza juhudi za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali na kuendelea kutoa fedha za maendeleo na za utafiti katika Taasisi hii ya TARI ili kufanikisha utekelezaji wa kazi na kwa kuwa Mhe. Rais amekuwa akiipa kipaumbele sekta ya kilimo kwa kuwa ndio uti wa mgongo wa Mtanzania, ni wajibu kuhakikisha maabara inapata ithibati na kutambulika kimataifa.

Mwenyekiti aliendelea pia kumpongeza Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde pamoja na Uongozi na wafanyakazi wote wa TARI kwa kusimamia kikamilifu ukarabati na ujenzi wa majengo ya Taasisi hiyo na kuendelea kufanya kazi kwa bidii.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...