Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhaj Hemed Suleiman Abdulla ameutaka Uongozi wa Kampuni ya Tigo/Zantel kuimarisha Miundombinu ya Mawasiliano ili kuweza kumudu ushindani wa kikanda na Kimataifa. 

Ameyasema hayo katika Iftar ya pamoja kati ya wadau, wateja na wananchi wa Zanzibar iliyoandaliwa na Kampuni ya Tigo/Zantel iliyofanyika katika Ukumbi wa Hotel ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege jijini Zanzibar.

 

Amesema kuwa Kampuni ya Tigo/zantel imekuwa ikijitahidi kufanya vizuri katika eneo la mawasiliano kwa kufikia asilimia 97% katika kutoa huduma za kimawasiliano kwa wateja na kuwataka kuzidisha uimara katika kazi zao mijini na vijijini ili kufikia malengo.

 

Aidha Alhajj Hemed ameutaka Uongozi wa Kampuni ya Tigo/Zantel kuzibiti viashiria vya vitendo viovu katika matumizi ya mitandao kama wizi,utapeli wa kutaka kujipatia mali kwa nguvu pamoja yale yote ambayo yanaathiri mila, silka na Tamaduni za wazanzibari na za watanzania kwa ujumla.

 

Makamu wa pili wa Rais amesema umefika wakati kwa Uongozi wa makampuni ya mawasiliano kuweka sheria na kanuni kwa wafanya kazi ambao watakwenda kinyume na maadili ya kazi zao sambamba na kuweza kuwachukulia hatua wale wote ambao wanarejesha nyuma maendeleo ya mawasiliano kwa wananchi.

 

Aidha ameyataka makampuni ya Masiliano Nchini  kushirikiana na TCRA na Mamlaka nyengine za mawasiliano katika kuzibiti matumizi mabaya ya mitandao ili watakaobainika hata kama ni watendaji wa kampuni zao waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

 

Sambamba na hayo Alhajj Hemed amesema Serikali itaendelea kutoa mashirikiano ya  hali ya juu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na za haraka na kuwata kuendeleza utamaduni wa kurudisha mrejesho wa faida kwa wateja wao utakaosaidia katika huduma mbali mbali za kijamii na kiuchumi.

 

Akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu, Afisa Mkuu wa Fedha Ndugu,INNOCENT RWETABURA amesema kampuni ya Tigo / Zantel imekuwa ikiimarisha huduma za mawasiliano siku hadi siku mijini na vijijini ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma zilizobora na kwa wakati.

 

Rwetabura amesema kuwa Kampuni ya Tigo/Zantel imeanzisha mfumo wa Kidijitali unaotumika mashuleni kwa kuhifadhia kumbukumbu, kutumika kwa kulipia ada, kutoa matokeo ya mitihani na kutumiwa na wazazi kwa kutoa na kupokea taarifa za watoto wao wanapokuwa katika masomo yao.

 

Aidha Rwetabura amewahakikishia wateja wao kuwa wataendelea kutoa huduma zilizo bora na za haraka zinazoendana na matakwa ya dunia ili wateja waweze kukidhi mahitaji yao ya mawasiliano kwa wakati stahiki.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...