Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb), amethibitisha kuwa mradi wa kupeleka mawasiliano ya simu vijijini ambao ni ujenzi wa minara 758, utakamilika ifikapo mwaka 2025.

Waziri Nape alitoa kauli hiyo tarehe 13 Machi, 2024 alipokuwa akitoa maelezo mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakati wa ziara katika eneo la ujenzi wa mnara wa mawasiliano ya simu katika Kijiji cha Itaga, Kata ya Misha, Tabora.

Waziri Nape alisema kuwa mikataba inayohusiana na mradi huo inatakiwa ikamilike ifikapo Februari 2025, na kuongeza kuwa kabla ya uchaguzi mkuu, minara yote itakuwa imewashwa na watu zaidi ya milioni 8 watakuwa wameunganishwa na mtandao.

Aliongeza kuwa, Serikali imepanga kuzindua zaidi ya minara 100 ambayo tayari imekamilika kwa awamu ya kwanza wakati wa sherehe za miaka 60 ya Muungano mwaka huo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Selemani Moshi Kakoso (Mb), aliitaka Serikali kuhakikisha kuwa Wizara itamaliza ujenzi wa minara hiyo kwa wakati, akisisitiza kuwa mawasiliano ni muhimu kwa jamii katika kuwezesha uchumi wa kidijitali.

Mhe. Kakoso pia alipongeza Wizara kwa jitihada zake za kuboresha huduma za mawasiliano nchini, pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika zoezi la operesheni Anwani za Makazi.

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Bi. Justina Mashiba, alisema kuwa Serikali kupitia mfuko huo imetoa ruzuku ya shilingi milioni 320 kwa Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL kwa ajili ya ujenzi wa minara 34 ya mawasiliano katika maeneo maalum nchini.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mhandisi Peter Ulanga, alisema kuwa minara mingi inayojengwa na shirika hilo inaunganishwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, na hivyo kasi ya mawasiliano imekuwa kubwa.

Minara hiyo 758 inajengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na kampuni mbalimbali za mawasiliano nchini, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua mradi huo tarehe 13 Mei 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Dodoma.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...