Na Mwandishi Wetu 

NAIBU  Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameahidi kuongoza kwa ufanisi usambazaji wa mitungi ya gesi takribani 10,000 iliyotolewa na Kampuni ya Taifa Gas hivi karibuni kwa ajili ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Mitungi hiyo iliyopokelewa hivi karibuni na Makamu wa Rais Dk. Phillip Mpango, ilitolewa na kampuni ya Taifa Gas ikilenga kuunga mkono kampeni ya kumtua mama kuni kichwani inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan. 

Kampeni hiyo inalenga kuwasaidia na kuwawezesha wananchi  kuifikia nishati hiyo kwa urahisi.

Kapinga ametoa ahadi hiyo katika kikao chake na maofisa waandamizi wa kampuni ya Taifa Gas wakiongozwa na Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Devis Deogratius walipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana.

Pamoja na kuipongeza kampuni hiyo kwa juhudi zake za kuunga mkono kampeni ya kumtua mama kuni kichwani Kapinga alisema ufanisi wa kampeni hiyo unategemea zaidi ushiriki wa wadau wengi zaidi kwa kuzingatia ukweli kwamba kampeni hiyo inalenga kuwafikia walengwa kote nchini.

 “Kama wizara, tumedhamiria kuhakikisha kwamba tunawafikia walengwa wote wanaostahili kufikiwa na kampeni hii kama ambavyo Rais Samia alivyokusudia. Kwetu imekuwa faraja kubwa kuona wadau kama Taifa Gas wapo nasi bega kwa bega kuhakikisha hilo linafanikiwa. 

"Pamoja na kusambaza mitungi hii ya gesi pia tutahakikisha elimu kuhusu nishati safi ya kupikia inawafikia walengwa kila wilaya na kila kata,’’ amesema Kapinga.

Aidha, Kapinga alitoa wito kwa kampuni ya Taifa Gas kuhakikisha kuwa inaongeza zaidi vituo vya kujazia gesi katika maeneo mbali mbali nchini, ili wananchi wengi zaidi waweze kufikiwa na huduma ya nishati hiyo kwa urahisi.

Kwa upande wake Deogratius amesema kuwa Taifa gas itaendelea kushirikiana na serikali katika kuimarisha kampeni ya matumizi ya nishati safi, huku akibainisha kwamba kampuni hiyo itaendelea na mkakati wake wa kupanua zaidi uwekezaji wake kwenye maghala yake nchini, ili kuihakikishia nchi usalama na upatikanaji wa nishati hiyo.

“Tunaelewa kuwa mabadiliko kuhusu matumizi ya nishati yanaendelea kuonekana na yatakuwa taratibu. Cha msingi ni kuweka mikakati ya kuongeza idadi ya watumiaji wa nishati safi nchini kutoka asilimia nane ya sasa,” amesema.Deogratius.   

Miongoni mwa maeneo ambayo yamelengwa na kampeni hiyo ni maeneo ambayo yameathirika kwa kiasi kikubwa na janga la ukataji wa miti kama vile mkoa wa Iringa na maneo mengine.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga (kulia) akipokea zawadi maalum ya kanga kutoka kwa Meneja Mkuu wa kampuni ya Taifa Gas, Devis Deogratius  wakati maofisa wa kampuni hiyo walipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...