Na Mwandishi wetu, Bariadi

TAMASHA kubwa la kimataifa la utamaduni na utalii linalojulikana kama Lake Zone Cultural and Tourism Festival limezinduliwa Bariadi Mkoani Simiyu.

Uzinduzi huo umefanywa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Yahaya Nawanda aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Anna Gidarya na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa Serikali, wadau wa utamaduni na Utalii kutoka katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na mikoa jirani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa ameipongeza kampuni ya Kilimanjaro One Travel and Tours kwa kubuni tamasha hilo la Utamaduni na Utalii kwa Kanda ya Ziwa na kuamua lifanyike katika Mkoa wa Simiyu.

Amesema utamaduni ni jambo kubwa la kujivunia na ni lazima uenziwe na kuendelezwa kwa nguvu zote kwa sababu ni urithi tuliopokea kutoka kwa babu zetu, hivyo na sisi hatuna budi kuuendeleza.

"Tamasha hili litasaidia sana kutangaza utamaduni wa mkoa wa Simiyu kupitia shughuli mbalimbali zitakazofanyika na hivyo kuufanya mkoa ufahamike zaidi ndani na nje ya nchi amesema Nawanda na kuongeza kuwa, "Nimearifiwa kuwa leo ni uzinduzi tu ili tupate kionjo kinachotarajiwa kufanyika mwezi wa saba 2024 ambapo kutakuwa na tamasha kubwa la siku tatu mfulululizo na litahusisha watu zaidi ya 7,000 wakiwemo washiriki wa maonyesho."

Amesema, tamasha hilo ni hatua kubwa kwani litapeleka fursa kwa washiriki kufanya biashara na kujifunza mambo mbalimbali na sekta ya utalii na utamaduni itakuwa kwa sababu wageni wote watakaokuja watapata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya mkoa wa Simiyu na kujionea vivutio mbalimbali vikiwemo vya utamaduni.


Aidha Dkt. Nawanda ametoa wito wa maandalizi ya tamasha hilo kubwa kufanyika mapema ili kupata washiriki wengi kutoka ndani na nje ya nchi.

Vilevile amewapongeza waandaaji kwa kuuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya SIta za kuhakikisha utamaduni wetu unatangazwa na kuufanya kivutio kikubwa cha watalii wa ndani na nje ya nchi.

“Napenda kutoa wito kwa wadau mbalimbali, wakiwemo watu binafsi, Mashirika, Taasisi na makampuni kujitokeza kudhamini tamasha hili kubwa katika Kanda ya Ziwa na nchini kwa ujumla ili lifanyike kwa ukubwa unaostahili na kukuza utamaduni na utalii wetu hapa nchini,”

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na waandaaji wa tamasha hili kuhakikisha linafanyika kila mwaka na kuwa chachu ya maendeleo kiutamaduni na kiuchumi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kilimanjaro One Travel and Tours Christina Emmanuel amesema kuwa hii ni mara ya kwanza kwa kampuni hiyo ambayo inajihusisha na masuala ya utalii na utamaduni kuandaa tamasha hilo ambalo wanaamini litakuwa na muitikio mkubwa kwa wakazi wa Simiyu na mikoa ya jirani.

“Tamasha hili linatarajiwa kufanyika mwezi wa saba na ninayo furaha kukufahamisha kuwa litafanyika kwa siku tatu mfulululizo Julai 5, 6 na kilele chake kitakua Julai 7 ambapo pamoja na mambo mengine tunategemea kuwa na maonyesho mbalimbali ya masuala ya utamaduni na utalii katika Uwanja wa Halmashauri na kuwavutia washiriki na watazamaji zaidi ya 7000 kwa siku hizo tatu huku pia kukiwa na vionjo mbalimbali ikiwemo ngoma inayohusisha makabila ya Wagika na Wagulu,” ameongeza Christina.

Ametoa wito kwa wafanyabiashara, makampuni, taasisi na mashirika kujitokeza na kuunga mkono kama njia moja wapo pia ya kuiunga mkono Serikali katika kuutangaza utamaduni na utalii wa nchi yetu.

Naye Afisa wa Baraza la Sanaa nchini (BASATA) Gabriel Awe amewasifu waandaaji kwa kuandaa tamasha hilo katika kuendeleza utamaduni na Utalii hapa nchini, akitoa wito kwa wadau wengine kuliunga mkono tamasha hilo kwa hali na mali.

“Ni tamasha kubwa la aina yake ambalo sisi kama Watanzania tunapaswa kujivunia kwani litaongeza chachu katika kukuza maendeleo ya utamaduni na utalii wetu".
 

Mkuu wa Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu, Anna Gidarya (katikati) akikata utepe kuzindua Tamasha la kimataifa la Utamaduni na Utalii maarufu kama Lake Zone Cultural and Tourism Festival linalotarajiwa kufanyika mapema Julai mwaka huu 2024. Uzinduzi wa Tamasha hilo linaloandaliwa na Kilimanjaro One Travel and Tours umefanyika leo Machi 16, 2024 Bariadi. Wengine kutoka kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Christina Emmanuel, Mkurugenzi, Mohamed Hatibu, Afisa Maendeleo ya Vijana, Zena Mchujuko, Afisa wa Baraza la Sanaa la Taifa, Gabriel Awe na wageni mbali mbali

 

 Mkuu wa Wilaya ya Itilima Anna Gidarya akizungumza wakati wa uzinduzi wa tamasha la  la kimataifa la Utamaduni na Utalii maarufu kama Lake Zone Cultural and Tourism Festival linalotarajiwa kufanyika mwezi Julai mwaka 2024.

 

 Mkurugenzi Mtendaji wa Kilimanjaro One Travel and Tours, Christina Emmanuel akizungumza wakati wa tukio hilo la uzinduzi.

 

Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Anna Gidarya akifurahia moja ya burudani wakati wa uzinduzi huo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...