Na Janeth Raphael - MichuziTv- Bungeni Dodoma.

Tathmini ya mwenendo wa hali ya uchumi inaonesha kuwa uchumi wa Tanzania uliendelea kuhimili changamoto za kiuchumi za kidunia kama vile mabadiliko ya tabia nchi na vita nchini Ukraine na ukanda wa Gaza, na kubadilika kwa sera za fedha nchini Marekani, ikiwemo kupandisha riba katika fedha zinawekezwa ndani ya nchi yao.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo (MB) ameyabainisha hayo leo wakati akiwasilisha mapendekezo ya Serikali ya mpango wa maendeleo ya Taifa wa mwaka 2024/2025 Leo Bungeni jijini Dodoma.

Profesa Kitila amesema Pato la Taifa liliongezeka kutoka shilingi trilioni 124.2 katika kipindi cha Januari – Septemba 2022 hadi kufikia shilingi trilioni 140.0 katika kipindi cha mwezi Januari hadi Septemba 2023. Pato la Taifa kwa bei za mwaka 2015 liliongezeka hadi shilingi trilioni 109.2 katika kipindi cha mwezi Januari hadi Septemba 2023 kutoka shilingi trilioni 103.7.

"Uchumi wa Taifa ulikua kwa asilimia 5.3 katika kipindi cha Januari – Septemba 2023 ukilinganisha na asilimia 5.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2022." - Amesema Prof. Kitila

Ukuaji huo ulichangiwa na jitihada mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya awamu ya sita ikiwemo: mikakati ya kukabiliana na athari za vita kati ya Ukraine na Urusi; uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya nishati, maji, afya, elimu, barabara, reli na viwanja vya ndege; kuongezeka kwa uzalishaji wa madini, hususan dhahabu na makaa ya mawe; na kuongezeka kwa mikopo katika sekta binafsi ambayo imechochea shughuli za kiuchumi.

Aidha Prof Kitila amesema Sekta zilizokua kwa kasi kubwa katika kipindi cha marejeo ni pamoja na: Fedha na bima (asilimia 16.0); uchimbaji madini na mawe (asilimia 10.2); umeme (asilimia 10.0); huduma nyingine ikijumuisha sanaa na burudani (asilimia 10.0); malazi na chakula (asilimia 8.9); na habari na mawasiliano (asilimia 7.9).

"Katika kipindi hicho Shughuli za uchumi zilizokuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa ni pamoja na kilimo (asilimia 24.8), ujenzi (asilimia 13.6), uchimbaji madini na mawe (asilimia 9.7), biashara na matengenezo (8.4), uchukuzi na uhifadhi wa mizigo (asilimia 7.2), na viwanda (asilimia 6.9)." - Prof. Kitila

Hata hivyo Waziri huyo amesema kipindi cha mwezi Januari, 2024 mfumuko wa bei nchini ulifikia asilimia 3.0 ikilinganishwa na asilimia 4.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2023 na mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 3.8 mwaka 2023 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 4.3 mwaka 2022.

"Kiwango hiki kipo ndani ya malengo ya kati ya asilimia 3.0 hadi 7.0. Hali hii imetokana na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na bajeti na kuanza kuimarika kwa upatikanaji wa mazao ya chakula katika masoko ya ndani na ya nchi jirani."
 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof Kitila Mkumbo (Mb,) akiwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2024/2025 katika Ukumbi wa Msekwa, Bungeni Dodoma tarehe 11 Machi, 2024.
 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa na Naibu Spika wa Bunge  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mussa Azan Zungu (Kushoto) wakifuatilia taarifa ya uwadilishwaji wa mapendekezo ya Serikali ya mpango wa maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2024/25 leo katika ukumbi wa Msekwa Bungeni jijini Dodoma.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...