Na Munir Shemweta, MSOMERA

Jumla ya viwanja 10,000 vinatarajiwa kupangwa na kupimwa katika sehemu ya eneo lililokuwa Pori Tengefu la Handeni awamu ya pili kwa ajili ya wakazi wanaohamia kutoka hifadhi ya Ngorongoro.

Hayo yamebainishwa tarehe 7 Machi 2024 na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda katika eneo linalotekelezwa mradi wa kupima viwanja na mashamba wakati wa ziara ya pamoja ya Mawaziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na ile ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwenye eneo la kijiji cha Msomera Handeni mkoa wa Tanga.

Mhe, Pinda amesema, kati ya viwanja hivyo viwanja 5000 ni kwa ajili ya makazi na 5000 ni mashamba. Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi viwanja 2500 vya makazi vitapimwa kwenye kijiji cha Msomera, viwanja 1500 kijiji cha Kitwai B (Simanjiro) na viwanja 1000 kijiji cha Sauyi (Kilindi).

Aidha, amesema hadi kufikia februari 28 mwaka huu jumla ya viwanja 5,882 vimepimwa sawa na asilimia 118 ya lengo la kupima viwanja 5000 katika maeneo ya upangaji yaliyopo vijiji vya Saunyi (Kilindi) na Msomera (Handeni).

Amebainisha kuwa, kati ya viwanja hivyo, viwanja 5,272 ni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi pekee na hivyo kuwa na ziada ya viwanja 610 ikilinganishwa na malengo ya upatikanaji viwanja 5000.

Mhe, Pinda ameweka wazi kuwa, zoezi la upimaji mashamba linaendelea katika kijiji cha Msomera ambapo hadi kufikia februari 28, 2024 jumla ya idadi ya mashamba 3,507 yamepimwa sawa na asilimia 70 ya lengo la kupima mashamba 5000 katika maeneo ya upangaji ya msomera, Saunyi na Kitwai.

"Ili kufikisha lengo la kupima mashamba yaliyobaki 1493 tunategemea kukamilika kazi ya uwandani ndani ya wiki mbili, kazi ya uandaaji wa mipangokina kwa ajili ya upimaji mashamba inaendelea". Alisema Mhe, Pinda

Mhe, Pinda alimshukuru Rais Mhe, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuiwezesha Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi vifaa alivyovieleza kuwa vimesaidia na vinaendelea kusaidia katika utekelezaji wa mradi katika eneo la kijiji cha Msomera na maeneo mengine.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe, Abdallah Ulega aliipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kazi kubwa na nzuri ya kufanikisha mipangpkina na hatimaye kupima mashamba na viwanja katika eneo la Msomera.

‘’Kazi imeonekana na tumeona kazi nzuri ambayo imekwisha kuanza na inaendelea ya upimaji viwanja na mashamba katika maeneo ya kilimo na mifugo katika eneo hili la Msomera ’’. alisema Ulega.

Hata hivyo, Mhe, Ulega amewataka watendaji wa sekta ya ardhi kutoa elimu kwa watumiaji ardhi na kusisitiza kuwa, jambo hilo lazima liwe endelevu ili kuepuka matumizi holela ya ardhi na kusisitiza kuwa lazima ardhi isimamiwe ipasavyo.

Utekelezaji wa mradi wa kupanga na kupima katika eneo la Msomera wilayani Handeni mkoa wa Tanga umefanikisha kuwaweka pamoja wageni wanaohamia kwa hiari kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na wenyeji waliokutwa kwenye eneo la pori tengefu kuisha pamoja na pasipo migogoro yoyote.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe, Abdallah Ulega (wa tatu kushoto) na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda (wa pili kushoto) wakimsiliza Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Hamdouny Mansoor kuhusu utekelezaji wa upangaji na upimaji viwanja katika eneo la B1 katika kijiji cha Msomera wilaya ya Handeni mkoa wa Tanga tarehe 7 Machi 2024.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe, Abdallah Ulega na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda wakioneshwa ramani ya eneo la utekelezaji upimaji viwanja katika eneo la B1 katika kijiji cha Msomera wilaya ya Handeni mkoa wa Tanga tarehe 7 Machi 2024.

Timu ya wataalamu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikiwa katika eneo la utekelezaji mradi wa upimaji viwanja katika eneo la B1 katika kijiji cha Msomera wilaya ya Handeni mkoa wa Tanga tarehe 7 Machi 2024.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe, Abdallah Ulega na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda wakiwasili eneo ulipofanyika mkutano wa wananchi waliohamia kutoka hifadhi ya Ngorongoro tarehe 7 Machi 2024.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe, Abdallah Ulega (wa pili kushoto) na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda (wa kwanza kushoto) pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Handeni Albert Msando (aliyesisima juu) wakishuhudia uondoaji wadudu kwa mifugo katika eneo la Josho la Mifugo katika kijiji cha Msomera wilaya ya Handeni mkoa wa Tanga tarehe 7 Machi 2024.

Sehemu ya wananchi waliohamia kutoka hifadhi ya Ngorongoro wakiwa katika mkutano wa Mawaziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika eneo la Msomera tarehe 7 Machi 2024.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe, Abdallah Ulega na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda wakiangalia mbuzi wa Mradi wa kikundi cha vijana wanaofanya unenepeshaji katika kijiji cha Msomera mkoa wa Tanga tarehe 7 Machi 2024. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...