NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

KATIKA Kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani, Wanaharakati wa jinsia wamefanya mdahalo,wenye lengo la kudai haki na usawa kwa kupinga uonevu kwa wanawake kwa kuunda mfumo huru unaotoa fursa sawa katika ujira,kumiliki mali na nafasi za kuwa viongozi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 01,2024 Mkurugenzi wa Shirika la WiLDAF Bi. Anna Kulaya amesema kuwa nchi haiwezi kuendelea kama wanawake wakiendelea kukandamizwa na kutoshiriki katika ngazi za maamuzi.

"Kwenye ngazi za maamuzi huko ndiko wanawake wangepaswa kuonesha uzoefu wao na ujuzi wao, wanawake wameonekana kwa muda mrefu wanapaswa kulea watoto, ukilea mtoto unafahamu tabia za watoto unafahamu chakula bora, hata hilo suala la utapiamlo lisingekuwepo". Amesema.

Amesema kuwa wanawake wengi hawamiliki rasmali kutokana na Sheria kandamizi ya mirathi inayozuia wanawake kumiliki ardhi jambo ambalo linazorotesha maendeleo ambapo ikirekebishwa jamii kubwa ya wanawake itafaidika na kuinuka kiuchumi.

Aidha Bi. Kulaya amesema kuwa asilimia mbili pekee kati ya asilimia mia moja ambayo ni ya wanawake viongozi katika ngazi ya vijiji,na ngazi ya vitongoji asilimia sita, na asilimia kumi na mbili katika ngazi ya mtaa.

"Haiwezekani nchi ikawa na wanawake wengi wengi alafu hawashiriki katika ngazi za uongozi, takwimu zinaonesha wanawake wapo wengi sana alafu hawashiriki katika ngazi za uongozi, lazima tuwe na jamii ambayo wanawake na wanaume wanashirikiana". Bi.Kulaya ameeleza.

Pamoja na hayo ametoa wito kwa vyama vya siasa kuunda mikakati mahususi wa mazingira ambayo yatasaidia wanawake waweze kuchaguliwa kuwa viongozi ili kuwa na uwiano sawa na kuchochea maendeleo.

Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Temeke Mariam Seif amesema kuwa changamoto inayowakabili wanawake wakati wa uchaguzi katika kipindi Cha kampeni ni suala la uchumi ambalo limekuwa kikwazo kwao katika kugombea ngazi mbalimbali za uongozi.

Nae, Mwenyekiti wa mtaa wa Machimbo kata ya Segerea Bi.Mariam Maticha amesema kashfa za uzushi katika kipindi cha uchaguzi hasa kwa wanawake imekuwa sababu kubwa ya kuwakwamisha wanawake kuwa viongozi kutokana na suala la mfumo dume.

MAADHIMISHO hayo ya wanawake yatafanyika Machi 08,2024 na yamebeba kauli mbiu isemayo"WEKEZA KWA WANAWAKE ILI KUHARAKISHA MAENDELEO" ambapo adhma kuu ni kuibua haki na usawa kwa jinsia zote.
Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...