# Wakumbushwa kuwa watendaji

Tunapoelekea Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa tarehe 8 Machi, 2024 kila mwaka, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imewajengea uwezo katika eneo la fedha watumishi wake ili kuwakumbusha kujiwekea akiba na kuwekeza kusikohitaji nguvu kubwa.

Mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam zilipo ofisi za Mamlaka baada ya wanawake wengi kuhitaji elimu ya fedha iliyopelekea uongozi wa Mamlaka kuridhia na kumuandaa mwezeshaji wa masuala hayo.

Mkurugenzi wa TFRA, Joel Laurent ametaka mafunzo hayo yawasaidie watumishi hao kuwa na fikra chanya ya kuweza kufikia dhana ya usawa kama inavyoshauriwa na viongozi wa kitaifa na kimataifa.

"Tuwe tunajiuliza endapo kuna mahala tunaona tumelala kidogo katika masuala ya kijinsia basi tuamke" amesema Laurent.

Ameeleza kuwa, ili mtu yeyote aweze kuwekeza anahitaji kuwa na uelewa juu ya namna ya kuwekeza hususan uwekezaji unaohusisha kununua hisa, kuweka amana, hatifungani na uwekezaji mwingine wote ili uweze kunufaika.

Akitoa mafunzo hayo, Mwezeshaji CPA, Emmilian Busara amesema ajira ni nzuri lakini zina ukomo na kuwakumbusha umuhimu wa kuwekeza na kuweka akiba itakayowawezesha kuendesha maisha yao mara baada ya ajira kukoma au kukutana na jambo litakalowatoa kwenye ajira.

CPA Busara, amewataka watumishi kuweka malengo ya juu katika mipango yao huku akifafanua kuwa mafanikio ya mtu yanatokana na kile anachokusudia kukipata moyoni mwake, pia aliwashauri kuwa na vyanzo tofauti vya mapato ili kimoja kikisumbua unakuwa na uhakika wa kuingiza kipato kupitia chanzo kingine na hivyo kupunguza msongo wa Mawazo.

"Huwezi kufanikiwa zaidi ya unavyowaza, jitahidi kuwaza mambo makubwa maana huwezi kufanikiwa zaidi ya unavyowaza" Busara alisisitiza.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, Victoria Elangwa aliwataka watumishi kuyaingiza mazuri waliyojifunza kwenye matendo na si kuyatia kapuni, amesema watumishi wamehamasika sana kwa elimu waliyoipata na kuwashauri vijana waliobahatika kujifunza elimu ya uwekezaji katika umri mdogo kutumia fursa hiyo itakayowapa uhuru wa kifedha katika Maisha yao.

Mwisho aliwataka watumishi ambao umri wa kati kutumia elimu hiyo kuanzia hapo walipo na kueleza itasaidia kubadilisha masuala fulani ya namna fedha yao inavyotumika kwa kuwekeza zaidi.
Mwezeshaji CPA Emmilian Busara akitoa elimu kwa watumishi wa TFRA  juu ya kuweka mipango, usimamizi wa Fedha na uwekezaji yaliyofanyika    katika ukumbi zilipo ofisi za Mamlaka Jijini Dar es Salaam
 

Viongozi Waandamizi wa Mamlaka, Mkurugenzi Mtendaji, Joel Laurent (kulia) na Mkurugenzi wa Huduma za Mamlaka, Victoria Elangwa wakifuatilia mada juu ya elimu ya Mipango, Usimamizi wa Fedha, na Uwekezaji kutoka kwa mwezeshaji CPA Emmilian Busara

 

Watumishi wa TFRA wakifuatilia mafunzo juu ya kuweka mipango, usimamizi wa Fedha na uwekezaji yaliyotolewa na mwezeshaji CPA Emmilian Busara katika ukumbi zilipo ofisi za Mamlaka Jijini Dar es Salaam

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...