UTOAJI Wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi inayotolewa bure kwa wasichana kuanzia miaka 9 hadi 14 kwa dozi moja pekee umefanikiwa kwa asilimia 95 tangu kuanza kutolewa kwake Aprili 22, 2024.

Hayo yameelezwa na Meneja wa Mpango wa Chanjo wa Taifa; Dkt. Florian Tinuga jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari yaliyolenga kuwajengea uwelewa zaidi kuhusu chanjo hiyo ya Human Papilloma Vaccine (HPV,)

“Tangu kuzinduliwa kwake mwezi Aprili mwaka huu wasichana walengwa asilimia 95 wamefikiwa na chanjo hii ambayo Wizara ya Afya kupitia Mfuko wa Taifa wa Chanjo ililenga kuwafikia na kuwapa chanjo wasichana 187,059 kutoka visiwani Zanzibar na 4,841,298 kutoka Tanzania Bara ambao wamefikisha umri wa miaka 9 hadi 14.” Amefafanua.

Aidha kuhusiana na mabadiliko ya dozi ya chanjo hiyo kutoka dozi mbili hadi moja Dkt. Tinuga ameeleza kuwa mwaka 2023 Kamati ya Kitaalam ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu Masuala ya Chanjo ilifanya utafiti na kujiridhisha juu ya ubora na usalama wa dozi moja ni sawa na dozi mbili katika kutoa kinga ya mwili dhidi ya kirusi dhidi ya kirusi cha HPV.

“Utafiti wa kisayansi kuhusu usalama wa dozi moja ni matokeo ya tafiti za kisayansi za ubora na usalama wa dozi moja kwa wasichana zilizofanywa na wataalam wetu pamoja na muongozo uliotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO,) mwaka 2022 ambalo pia lilithibitisha ubora na usalama wa chanjo moja na kutoa uamuzi kwa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa katika kutoa dozi moja ya kuwakinga wasichana dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi…” Amesema.

Amesema kuwa mwitikio wa wasichana wa umri lengwa kwa ajili ya kumkinga binti dhidi ya maambukizi ya saratani ya mlango wa kizazi ni mkubwa kutokana na ushirikiano na wadau mbalimbali hususani Wizara ya Elimu pamoja na wazazi na walezi kwa kuwa chanjo hizo hutolewa shuleni na katika vituo vya huduma za chanjo katika vituo vya Afya.

Amesema saratani ya mlango wa kizazi husababishwa na kirusi cha papilloma na huambukizwa kwa njia ya kujamiiana na wanaume ndio hubeba kirusi hicho na mwanamke kupata madhara zaidi huku dalili zake zikiwa ni pamoja na kupata hedhi isiyo na mpangilio maalum na kutokwa na uchafu au damu ukeni huku Mikoa ya Kilimanjaro, Dar es Salaam na Mwanza ikiongoza kwa saratani hiyo.

Imeshauriwa kuwa ni vyema wasichana wa umri wa miaka 9 hadi 14 kupatiwa chanjo hiyo kwa kuwa imethibitika kisayansi katika umri huo mwili una uwezo wa kujitengenezea kinga ya kutosha, kuepuka ngono katika umri mdogo pamoja na kufanya uchunguzi kila baada ya miaka mitatu hadi mitano ili kufahamu dalili za awali na kuwahi tiba.
 

Meneja wa Mpango wa Chanjo wa Taifa Dkt. Florian Tinuga (kulia,) akitoa mada wakati wa mkutano huo na kueleza kuwa chanjo ya HPV ni salama kwa kinga mwili dhidi ya kirusi cha papilloma kinachosababisha saratani ya mlango wa kizazi. 

Matukio mbalimbali wakati wa mkutano huo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...