Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Dkt. Sheikh Abubakar Zubeir bin Ali Mbwana ameitaka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni, (BRELA) kutoa elimu kwa watu waielewe na kufaidika na huduma inazozitoa.

Sheikh Zubeir ametoa rai hiyo jana tarehe 3, Aprili, 2024 katika hafla ya Iftar iliyoandaliwa na BRELA kwa wadau wake iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali na kufanyika Jijini Dar es Salaam.

Ameeleza kuwa, wapo watu waliofungua kampuni bila kufahamu jinsi ya kusimamia, BRELA iendelee kufungua milango ili watu wengi wapate kuifahamu taasisi na inachokifanya ili kuwasaidia kufanya biashara kwa mujibu wa sheria.

“Taasisi itoe elimu kuhusiana na masuala ya BRELA kwa kuwa wapo wengi huitaja Wakala lakini hawajui inafanya nini, hivyo ni muhimu kuwaelimisha ili watafahamu huduma zinazotolewa, jinsi ya kuzipata na umuhimu wake”. Alisema Sheikh Zubeir

Akieleza umuhimu wa elimu Sheikh Zubeir amefafanua kuwa mtu huweza kuharibikiwa na mambo mengi asipokuwa na elimu huku akitanabaisha kuwa ujinga ni aibu na hakuna anayeukubali na akauridhia.

Katika hatua nyingine Sheikh Zubeir amempongeza Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa kwa kuandaa iftar kwa mara ya kwanza na kushukuru kwa kumwalika pamoja na wadau wengine kuwa watu wa kwanza kushiriki katika tukio hilo, na kumsihi kuwa zoezi hilo liwe endelevu.

“Awali nilimuuliza Bw. Nyaisa hii ni Iftar ya ngapi kufanya, akanieleza kuwa hii ndio mara ya kwanza zoezi kama hili linafanyika, nampogeza sana kwa kuandaa n ani Imani yangu kwamba mtaendelea kufanya vizuri zaidi” Amesema Sheikh Zubeir.

Awali akimkaribisha Mufti katika hafla hiyo, Bw. Nyaisa, alimshukuru Mufti na Sheikh Mkuu kwa kukubali kushiriki katika hafla ya Iftar ya kwanza kwa BRELA na kuahidi kuboresha zaidi sambamba na kuwakumbuka watu wenye uhitaji.

BRELA imeandaa iftar hiyo kwa mara ya kwanza kwa lengo la kuwa karibu na wadau ambapo Mhe.Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dkt. Sheikh Abubakar Zubeir bin Ali Mbwana alikuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo.

Pamoja na hafla hiyo BRELA inatarajia kurudisha kwa jamii kwa watu wenye uhitaji.
 

Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Dkt. Sheikh Abubakar Zubeir bin Ali Mbwana

Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa

 

 

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...