Na Mwandishi wetu

CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimetoa msaada wa vitu mbalimbali vikiwemo viti mwendo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wa shule ya sekondari ya Jangwani jijini Dar es Salaam.

Msaada huo umekabidhiwa leo Aprili 18,2024 shuleni hapo na Mkurugenzi wa Taaluma wa CBE, Dkt. Shima Banele, katika hafla fupi iliyowashirikisha wanafunzi zaidi ya 110 wa shule hiyo wenye mahitaji maalum.

Akizungumza maara baada ya kukabidhi msaada huo, Dkt.Banele amesema chuo hicho kimejenga utamaduni wa kusaidia shule hiyo kila mwaka kwani inapokea wanafunzi wenye mahitaji maalum wanaosoma elimu jumuishi.

Dkt. Banele amesema chuo hicho kitaendelea kusaidia shule hiyo ili wanafunzi wenye mahitanji maalum waweze kusoma kwa bidii na kutimiza ndoto zao siku za baadaye.

Amesema kila mwaka chuo hicho kimekuwa na utamaduni wa kuchukua sehemu ya wanachopata na kurejesha kwenye makundi mbalimbali ndani ya jamii kama sehemu ya kutambua mchango wake kwa chuo.

Aidha amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari kwani wanafunzi wengi walikuwa wanashindwa kwenda shule kutokana na kukosa ada sasa wanaweza kupata elimu yao.

Pia amepongeza hatua ya serikali kuweka elimu jumuishi ambapo wanafunzi wenye mahitaji maalum wamekuwa wakichanganywa na wale ambao hawana changamoto yoyote.

Amewataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao na kuachana na fikra za kujiona wanyonge kwani wakijiamini wanaweza kufaulu vyema kwenye masomo yao na kufanya vizuri kwenye elimu ya vyuo vikuu.

“Mnaweza kuwa na changamoto ya maumbile lakini ubongo wenu unafanyakazi vizuri kwa hiyo msifikirie kwamba hamuwezi, mnaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa jamii kama mtajibidisha na mkafaulu vizuri,” amesema

“Mtakapomaliza sekondari mkafaulu vizuri na kwenda vyuo vikuu mkimaliza hangaikeni kutafuta ajira kwasababu mnauwezo wa kufanyakazi kama wengine. Kila mtakapoona nafasi za ajira pelekeni wasifu wenu,” amesema.

Aidha, amewataka kuishi kwa upendo na kupeana moyo kwenye masomo yao ili waweze kufanya vizuri kwenye masomo yao na kukua kitaaluma badala ya kukandamizana kwa uchoyo na chuki.

“Mimi leo hapa namwakilisha Mkuu wa chuo cha CBE lakini kwa nafasi yangu pale ni Mkurugenzi wa taaluma sasa kama mimi nimeweza kufika nilipo kwa sasa kwanini kesho usiwe wewe. Kwa hiyo unatakiwa kuanza kufikiria kesho yako leo hii na ninaamini mtafanikiwa sana mkijituma,” amesema

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa shule hiyo, Paulina Aweda, amesema shule hiyo inawanafunzi 110 wenye mahitaji maalum na wanasoma masomo yote kama walivyo wanafunzi ambao hawana changamoto yoyote.

Amepongeza serikali kwa kuweka mazingira mazuri kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wanasoma bila vikwazo vyovyote na kwamba wamekuwa wakifanya vizuri kwenye mitihani yao ya mwisho ya kitaifa.

Amesema wanafunzi hao wenye mahitaji maalum wamekuwa wakipatiwa chakula, malazi na mahitaji mengine yote wanapokuwa shuleni hapo hali ambayo imewawezesha kufanya vizuri kitaaluma.

“Tunabahati ya kuwa na waalimu wa kutosha waliosomea elimu maalum ya kufundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa hiyo serikali imewafikiria kwa kiwango kikubwa wanafunzi wenye mahitaji maalum,” amesema.
 

Mwakilishi wa Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE),   Dkt. Shima  Banele ambaye ni Mkugenzi wa Taaaluma wa chuo hicho akimsukuma mwanafunzi kwenye kiti mwendo (wheelchair) walipokwenda kutoa msaada wa viti hivyo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wa shule ya sekondari Jangwani jijini Dar es Salama leo Aprili 18,2024.

 

Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Jangwani, Dar es Salaam Paulina Aweda (kulia) akionyesha tuzo ambayo amepewa leo Aprili 18,2024 na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kutambua mchango wa shule hiyo kutunza na kufundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wakati walipowatembelea shuleni hapo na kuwapa zawadi mbalimbali vikiwemo viti mwendo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...