Na Mwandishi Wetu,Same

KATIBU Tawala wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Upendo Wella amesema katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimefanikiwa kusimamia masuala ya muungano kwa ufanisi mkubwa.

Hiyo imesababisha kuimarika kwa utaifa, umoja, amani, utulivu, na hali ya maisha ya wananchi kutokana na ukuaji wa uchumi wa pande zote mbili za Muungano.

Wella ametoa kauli hiyo alipowaongoza wananchi katika upandaji miti ikiwa ni shamshara za sehemu ya sherehe za kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Zoezi hilo lilifanyika leo katika Kata ya Kisima, wilayani Same.

Aidha,amewahimiza wananchi wa wilaya ya Same kuendeleza utamaduni wa kupanda miti sehemu mbalimbali, hasa kipindi hiki ambacho mvua zinanyesha kwa wingi, ili miti iweze kustawi vyema na kuepukana na hali ya ukame.

Pia amewaomba walimu wote kuhakikisha kila mwanafunzi anapanda mti katika mazingira ya shule na kusimamia ukuaji na utunzaji wa mti huo, pamoja na kuhimiza upandaji miti majumbani, katika taasisi za serikali na zisizo za serikali, ili baadaye wilaya iwe na rutuba nzuri ya miti.

Katibu huyo pia amewaalika wananchi kushiriki katika mkesha wa kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar utakaofanyika tarehe 25, ambapo kutakuwa na matangazo ya moja kwa moja ya hotuba ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia channel ya TBC.

Amesema kwamba Aprili 26 ndio itakuwa kilele cha Siku ya sherehe za Muungano, wananchi watashiriki katika majadiliano ya masuala mbalimbali yanayoweza kujenga taifa.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...