Baadhi ya Wafanyakazi wa Barrick wakishiriki zoezi la kupanda miti katika hospitali ya jiji la Arusha.
Wafanyakazi wa Barrick wakiwa na wafanyakazi wa hospitali ya Arusha baada ya kushiriki zoezi la kupanda miti kwenye hospitali hiyo baada ya kushiriki zoezi la kupanda miti.
Mwenyekiti wa Bodi ya OSHA, Dk. Adelhelm Meru alipotembea banda la maonesho la Barrick.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, akitembelea banda la Barrick Tanzania kupitia migodi ya Bulyanhulu, North Mara na Buzwagi.

Na Mwandishi Wetu.

Elimu ya afya na usalama mahali pa kazi inaendelea kuwafikia wananchi mbalimbali ambao wanatembelea banda la maonesho ya kampuni ya dhahabu ya Barrick kupitia migodi yake ya Bulyanhulu, North Mara na Buzwagi kwenye maonesho ya Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) yanayoendelea mkoani Arusha.

Mbali na elimu hiyo pia wafanyakazi wa Barrick wameshiriki katika programu za kupanda miti maeneo mbalimbali kwa ajili ya utunzaji wa mazingira kwendana na kauli mbiu ya maonesho ya mwaka huu inayohimiza utunzaji wa mazingira kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mratibu wa Mazingira wa Barrick (Safety Coordinator), Hassan Kallegeya ameeleza baada ya kuongoza zoezi la kupanda miti kuwa katika maonesho ya mwaka huu mbali na kutoa elimu ya usalama mahali pa kazi wameshiriki pia kupanda miti kwendana na kauli mbiu ya OSHA ya maonesho hayo mwaka huu isemayo athari za mabadiliko ya tabia nchi katika usalama mahali pa kazi.

Alisema athari za mabadiliko ya tabia nchi, zinamuathiri kila mmoja hivyo mbali na kufundisha usalama pia wanazo programu za utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kukabiliana na majanga yatokanayo na mabadiliko hayo.

Barrick imekuwa ikitekeleza kampeni ya ‘Journey to zero’ ambayo inalenga kuhamasisha afya na usalama kwa wafanyakazi wake ambayo sasa inapelekwa kwa wadau wengine wote kwenye jamii.

“Kampeni yetu ya 'Journey to Zero' inalenga kuhakikisha wafanyakazi wote wa kampuni wanakuwa salama wakati wote wanapokuwa kazini hadi wanaporudi nyumbani hivyo tumehakikisha kampeni hii inavuka mipaka hadi nje ya kampuni kuhakikisha jamii nzima inakuwa salama na ndio maana tunaendelea kuendesha mafunzo ya usalama kwa jamii ili kuhakikisha jamii yote inakuwa salama”. alisema.

Wakati huohuo banda la maonesho la Barrick limekuwa likitembelewa na viongozi mbalimbali na Serikali na wananchi ambao wameweza kuona vifaa mbalimbali vya kisasa vya usalama na udhibiti wa majanga mbalimbali ikiwemo moto pia kupata mafunzo kutoka kwa wataalamu mbalimbali wa usalama.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Paul Makonda ni miongoni mwa wageni walioteembelea banda la Barrick katika maonesho hayo na kupongeza kampuni kwa kuwekeza katika vifaa vya usalama vya teknolojia ya kisasa sambamba na kuwa na programu za kutoa elimu ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi kwenye jamii nje ya migodi yake.

Usalama ni sehemu muhimu ya DNA ya Barrick.Katika kudhihirisha hilo migodi yake nchini Imekuwa ikishinda tuzo mbalimbali zinazotolewa na taasisi za nchini na za nje.Mwaka jana Barrick Tanzania ilinyakua tuzo sita za OSHA.) Mgodi wa Dhahabu wa Barrick Bulyanhulu, ulishinda tuzo kubwa ya mshindi wa jumla.

Mbali na ushindi huo mkubwa, Bulyanhulu, pia ilinyakua tuzo ya uandaaji Ripoti Bora ya Tathmini ya Hatari katika uchimbaji madini na mshindi Bora wa tuzo ya Usalama na afya (OHS) katika sekta ya madini.

Kwa upande wake, Barrick North Mara, ilishinda tuzo za juu katika: Kujali zaidi Wafanyakazi wenye Mahitaji Maalum na utekelezaji sera bora ya Usalama mahali pa kazi (OHS). Pia ilikuwa mshindi wa pili kwa washindi wa jumla wa sekta ya Madini. Mgodi wa Buzwagi pia ulishiriki maonesho hayo na kunyakua tuzo ya utekelezaji Mpango Kazi Bora wa Usalama na Afya mahali pa kazi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...