Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Kanda ya Magharibi, limewapatia elimu wanafunzi 5,000 katika shule za sekondari 20 za Manispaa ya Tabora kuhusu kazi za Baraza, taratibu na miongozo mbalimbali ya kujiunga na vyuo vya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini.

Akizungumza na baadhi ya wanafunzi, Meneja wa NACTVET Kanda ya Magharibi, Bi. Faraja Makafu amesema, kampeni hiyo imelenga kuondoa changamoto wanazopata wanafunzi wakati wa kuomba kujiunga na vyuo mbalimbali vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi mara baada ya kuhitimu masomo yao ikiwemo changamoto ya kudahiliwa katika vyuo na programu zisizo na ithibati ya Baraza.

“Uzoefu wetu na maoni toka kwa wadau wetu mbali mbali umetufanya tuanzishe kampeni ya Kanda kwa kanda ili kuwasaidia wanafunzi kufanya maamuzi na machaguo sahihi wakati wa kuomba vyuo. Wanafunzi wanapaswa kuomba udahili kwa usahihi na kwa kuzingatia taratibu na miongozo iliyowekwa ili waweze kutimiza ndoto zao”, alitamatisha Bi. Faraja.

Aidha, Meneja huyo wa Kanda amewataka wanafunzi hao kusoma kwa makini kitabu cha mwongozo wa udahili ambacho kinapatikana katika tovuti ya Baraza (www.nactvet.go.tz) kwani kina maelezo ya kina ya hatua kwa hatua hadi kukamilisha udahili wa wanafunzi katika vyuo vya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi.

Kwa upande wao, wanafunzi hao kwa nyakati tofauti wameshukuru hatua ya NACTVET kuanzisha zoezi la kuwapatia wanafunzi Elimu hiyo muhimu kwao na kuahidi kuwa mabalozi wazuri kwa wengine kwa kuwaeleza umuhimu wa kuzingatia taratibu na miongozo pindi watakapoamua kujiunga na vyuo mbalimbali.

Kampeni ya uelimishaji wanafunzi wa shule za sekondari za Kanda ya Magharibi, mkoani Tabora imeanza tarehe 22 Aprili, 2024 na itafikia tamati mnamo tarehe 1 Mei, 2024, ambapo miongoni mwa shule zilizokwishatembelewa ni pamoja na Shule ya Sekondari ya Wavulana Milambo, Shule ya Sekondari ya Wasichana Tabora, Shule ya Sekondari Themi Hill, Shule ya Sekondari ya wavulana Tabora, Shule ya Sekondari Ipuli, Shule ya Sekondari Cheyo, Shule ya Sekondari Isevya na Shule ya Sekondari Mihayo.

NACTVET ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge, Sura ya 129 na Marekebisho Madogo Na.4 ya mwaka 2021, kwa lengo la kurekebu Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini. Fasiri ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi ina nasibishama “Elimu na Mafunzo yanayotolewa kwa wanachuo kwa misingi ya ujuzi na umahiri (CBET), ili kuwajengea uwezo wahitimu kutekeleza majukumu yao yanayohitaji kiwango cha juu cha ujuzi, maarifa, uelewa na weledi kuwawezesha kutimiza wajibu wao kwa ufanisi na tija katika maeneo ya taaluma walizosomea”.

NACTVET ina jumla ya kanda nane zilizoanzishwa kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wadau. Kanda hizo ni ni pamoja na Kanda ya Mashariki Dar es salaam, Kanda ya Kati Dodoma, Kanda ya Magharibi Tabora, Kanda ya Ziwa Mwanza, Kanda ya Kusini Mtwara, Kanda ya Kaskazini Arusha, Kanda ya Kati Dodoma pamoja na Ofisi ya Zanzibar.
 

Meneja wa NACTVET Kanda ya Magharibi Tabora Bi. Faraja Makafu akitoa Elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mihayo
 

Afisa Uthibiti wa NACTVET Kanda ya Magharibi Tabora, Bw. Mohamed Kaunasa akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana  Milambo.
 

 Meneja wa NACTVET Kanda ya Magharibi Tabora, Bi. Faraja Makafu akitoa zawadi kwa  mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kamazima.


 

Picha za matukio mbalimbali katika utoaji elimu wa NACTVET.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...