Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah amesema Tanzania inaunga mkono harakati za kuwezesha usafirishaji wa bidhaa kwa huru na haraka mipakani kwa kuzingatia usalama wa Nchi ili kukuza uchumi wa kanda nzima na Barani Afrika.

Dkt. Abdallah ameyasema hayo Aprili 2, 2024, wakati akichangia mjadala wakati wa Kongamano la Usimamizi wa Mipaka katika Ufanyaji Biashara Mpakani linalofanyika Nairobi, Kenya kuanzia Aprili 2 -4, 2024 likijumuisha wajumbe kutoka Kenya, Uganda, Ethiopia, Sudan Kusini, Somalia, Tanzania na Afrika Kusini .

Amebainisha kuwa Kongamano hilo linatarajiwa kufikia makubaliano muhimu kuhusu mtengamano wa biashara na biashara mipakani yanayolenga kuboresha mazingira ya biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi katika kanda.

Aidha, Dkt. Abdallah amesisitiza kuwa ushirikiano wa kikanda na diplomasia ya kiuchumi ni muhimu na ni ahadi iliyotolewa na viongozi wa Tanzania na Kenya walipokutana jijini Dar es Salaam July 26, 2023. Viongozi hao walisisitiza umuhimu kukutana mara kwa mara ili kujadili na kutatua changamoto za biashara mipakani.

"Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Mheshmiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imedhamiria kufungua Nchi kupitia diplomasia ya uchumi ambayo msingi wake mkuu ni mtengamano wa biashara za kikanda na kimataifa". Amesisitiza Dkt Abdallah.

Akizungumza katika Kongamano hilo, amesisitiza kuwa Tanzania ni Baba wa Amani na mtetezi wa muda mrefu wa amani na usalama katika Kanda ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla huku ikiwa inajali masuala ya haki za binadamu na utu wa raia wake.

Naye Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala,alielezea juhudi za Tanzania katika kuboresha usimamizi wa mipaka kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kuboresha ufanisi wa mipaka na ufanyaji biashara.

Aidha, Dkt Makakala alitaja mifumo inayotumiwa na Tanzania ikiwemo Mfumo wa Uhamiaji wa Kielektroniki ulioanzishwa mwaka 2018, Mfumo wa Usimamizi wa Mipakani kwa njia ya Mtandao unaowezesha kubadilishana data na mawasiliano kati ya vituo tofauti vya mipakani.

Vilevile amebainisha kuwa Tanzania inafanya kazi na nchi jirani katika kuhakikisha harakati nzuri ya watu na biashara katika mipaka ya pamoja kwa kujumuisha timu za pamoja za uhamiaji katika vituo vya vya huduma za pamoja za mipakani na kamati za kikanda zinazoshughulikia changamoto za pamoja.Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...