*Ampongeza Rais Dkt. Samia kwa kutenga sh. trilioni 8.18 sekta ya nishati

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kutenga fedha za kutekeleza miradi ya nishati ambapo katika kipindi cha miaka mitatu zaidi ya shilingi trilioni 8.18 zilitolewa.

“Maono na maelekezo yake kuhusu usimamizi wa sekta hii yamekuwa na mchango mkubwa katika ufanisi wa shughuli za sekta, katika hili, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuweka kipaumbele kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya nishati.”

“Katika kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa umeme nchini, tayari nchi yetu imeanza kutumia umeme wa bwawa la Julius Nyerere Hydropower Project (JNHPP). Huu ni ushindi na kielelezo tosha kwamba Mama yupo kazini.”

Ametoa pongezi hizo leo jioni (Ijumaa, Aprili 19, 2024) wakati akifunga Maonesho ya Wiki ya Nishati yaliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

Waziri Mkuu amelipongeza Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kwa kuweza kuzalisha umeme zaidi ya mahitaji yaliyopo sasa. “Leo tarehe 19 Aprili, 2024 uzalishaji wa umeme ni mkubwa. Shirika letu la TAMESCO limemudu kuzalisha umeme zaidi ya mahitaji tuliyonayo na bwawa la Julius Nyerere Hydropower Project limeanza kazi na tayari megawati 235 ziko kwenye mfumo.”

Ameitaka Wizara hiyo iweke mkakati wa kuhakikisha maonesho hayo yanakuwa endelevu ili Waheshimiwa Wabunge waweze kupata fursa ya kuwasilisha hoja zao mahsusi na kutatua kero za wananchi wanaowawakilisha.

Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya washiriki wa maonesho hayo ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita, Waziri Mkuu ameitaka Wizara hiyo ione uwezekano wa kuandaa maonesho kama hayo katika ngazi ya Mikoa na Halmashauri. “Wakurugenzi wa Kanda na Mameneja wa Mikoa na Wilaya mko hapa. Nendeni mkae na muangalie jinsi ya kutekeleza jambo hilo,” amesisitiza.

Ameitaka Wizara hiyo iweke mkakati wa kuhakikisha wananchi wote wanapata ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusu fursa zinazopatikana kutokana na miradi inayotekelezwa na sekta ya nishati. “Pamoja na kuyaleta maonesho hapa Bungeni, kuna haja ya kupeleka maonesha kama haya kwenye maeneo ya katiati ya mji ili muweze kuwafikia wananchi wengi zaidi na kujibu hoja zao,” amesema.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wadau mbalimbali walioshiriki maonesho hayo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameipongeza TANESCO kwa kuendelea kufanya kazi nzuri ya kuhakikisha wananchi wanapata nishati ya umeme.

Naye, Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson amesema sekta ya nishati ni kati ya sekta mtambuka kwa sababu inalisha sekta nyingine nyingi na ikitikisika, inatikisa na maeneo mengine pia.

Amesema pamoja na utoshelevu wa umeme kwenye gridi ya Taifa, ili kuwe na maendeleo bado nchi inahitaji umeme wa kutosha na hasa kwenye viwanda na siyo kuwasha taa za majumbani.

Ameitaka Serikali itafute njia ya kutumia vizuri maji yanayotoka kwenye bwa la JNHPP ili yaweze kuwanufaisha wananchi wanaoishi maeneo ya jirani na bwawa hilo. “Bwawa limejaa kwa hiyo Serikali ihakikishe maeneo ya jirani yanapata maji ya kutumia. Tuanzishe gridi ya maji kama ilivyo kwenye gridi ya umeme. Kule chini tutengeneze njia ya kutunza maji kwa ajili ya matumizi ya umwagiliaji na mifugo,” amesema.

Naye, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema ushiriki wa mwaka huu umevunja rekodi kwani watu zaidi ya 480 walitembelea maonesho hayo ambapo 267 walikuwa ni Waheshimiwa Wabunge.

Ameyataja maeneo ambayo washiriki walikuwa wakiulizia zaidi ni umeme, nishati ya jua, nishati jadidifu, nishati safi ya kupikia, mafuta na gesi.

Amesema ili kujenga uelewa mpana kwa wananchi, wanapanga kuandaa kongamano maalum juu ya gesi asilia ambalo linatarjiwa kufanyika Mei, mwaka huu.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...