Na Mwamvua Mwinyi, Pwani April 17


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza TARURA, TANROADS na TAZARA kushirikiana kufanya ukarabati katika maeneo yote yaliyopata athari za mvua zilizosababisha mafuriko Rufiji na maeneo mengine nchini .

Ameeleza, hatua hiyo itaenda sambamba wakati Serikali inasubiri kumalizika kwa mvua ili iweze kufanya ukarabati mkubwa.

Waziri Mkuu ametoa wito huo (Jumanne, Aprili 16, 2024) wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Chumbi, wilayani Rufiji, mkoani Pwani ambako alikwenda kukagua athari za mafuriko kwenye eneo hilo.

Aidha Majaliwa amewataka wananchi waliokumbwa na adha ya mafuriko waendelee kuwa watulivu wakati Serikali ikiendelea kuratibu utoaji wa misaada kwenye maeneo yaliyoathirika.

"Hadi sasa waathirika 740 wako kambini,:Barabara ya Mkongo hadi Utete na ile ya kutoka Mloka Mkongo zote zimeathirika"

" Tunafanya kazi ya kurejesha mawasiliano ili wananchi waweze kupata huduma muhimu,” alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu ambaye aliwasili Ikwiriri, Rufiji akitokea Mlimba, Morogoro aliwaomba wananchi hao waendelee kutulia kwani serikali iko nao na itaendelea kuwahudumia hadi hali yao irejee katika hali ya kawaida.

“Naomba mpokee salamu za pole kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunatambua kuna watu wamepoteza mali na wengine mifugo,” alieleza.

Majaliwa aliwataka watendaji wa vijiji waendelee kubaini maeneo mapya ya kuishi ambayo yatatumika kuhamisha kaya zilizoathirika.

“Watendaji wa vijiji tuainishe maeneo mapya ya kwenye miinuko ili baadaye watu waweze kuhamishiwa huko,” alisema.

Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jaffo, Naibu Waziri wa Nchi (OWM-SBU) Bi. Ummy Nderiananga, Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi na watendaji wengine.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...