Na Mwandishi Wetu,Dodoma.


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amepokea msaada wa 13.7m/- kutoka kwa wanachama wa kundi sogozi(WhatsApp) liitwalo Viongozi Tanzania.

Akipokea msaada huo katika hafla hiyo iliyofanyika jana ofisini kwake Mei 6,2024,mjini Dodoma ,Dkt Yonazi amewashukuru wanachama wa kundi hilo kwa kujitoa kwao kwenda kwa waathirika hao wa maporomoko ya udongo, tope, mawe na magogo kutoka mlima Hanang mkoani Manyara yaliyotokea mwishoni mwa mwaka 2023.
Dkt.Yonazi amesema msaada huo,pamoja na misaada ya wasamalia wengine inaunga mkono jitihada za serikali zinazoendelelea katika kurejesha hali ya kawaida kwa waathirika hao ikiwemo kujengea nyumba 108, ili wanaendelee kujitafutia riziki na kujiletea maendeleo yao.

Aidha, Dkt. Yonazi ametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kuwa na desturi ya kuwakimbilia wahitaji pale ambapo wanapata athari za majanga mbalimbali.

"Tunawashukuru wenzetu wa kundi la Viongozi Tanzania kwa uzalendo waliouonesha kwa ajili ya mchango huu mkubwa walioutoa, niwaombe Watanzania wenzangu tuzidi kushikana mkono hasa nyakati hizi ambapo sehemu nyingi nchini yametokea majanga mbalimbali,hivyo ni  jambo jema kuendelea kushirikiana kuwasaidia ndugu zetu, "alisema Dkt. Yonazi

Wajumbe wawili wa kundi hilo ambao ni Ndg.Benjamin Thompson, ambaye ndiye Mratibu Mkuu wa kundi hilo, pamoja na Mhandisi Archard Kato,ambaye ni mmoja wa Wanachama wa kundi hilo, waliwawakilisha wanachama wengine zaidi ya 600 walioko kwenye kundi hilo, ambao ni viongozi mbalimbali wa serikali,viongozi wa taasisi za umma,viongozi wa sekta binafsi,wahadhiri na viongozi wa vyuo vikuu,viongozi wa vyama vya siasa,viongozi wadiaspora n.k

Bw.Thompson alisema michango hiyo ilikusanywa kutoka kwa wanachama 145 tu kati ya wote walioko kwenye wa kundi hilo, ambao ndio waliweza kuchangia kwa wakati huo.
"Mkusanyaji wetu alikuwa ni Zamaradi Kawawa,ambaye alifanya kazi nzuri sana na kwa uaminifu mkubwa.Baada ya kumaliza kazi hiyo,tulikubaliana kwamba aweke pesa hizo kwenye akaunti ya maafa iliyopo chini ya ofisi ya Waziri Mkuu,na aliweka pesa hizo Desema 27,2023.Sasa hili lililofanyika hapa leo lilikuwa ni kukabidhi tu karatasi ya malipo yaani pay in slip",alisema Bw Thompson.

Naye Mhandisi Kato,  ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya kutengeneza mvinyo ya Alko Vintages iliyopo Dodoma, alisema wanachama wa kundi hilo wameguswa na janga hilo la Hanang na hivyo kuona umuhimu wa kutoa michango hiyo katika kuunga mkono juhudi za serikali za kukabiliana na majanga kama hayo.
"Tunakuahidi kwamba tutaendelea kuisaidia serikali kwa kidogo tulicho nacho katika kukabiliana na athari za majanga kama haya,na tungependa kuona hili jambo linaenea kwa watanzania wengi,yaani hata kabla ofisi yako haijafika au serikali haijafika, angalau watanzania wenyewe wawe wanafanya jambo la mwanzo kwa uzalendo wao katika kukabiliana na mambo hayo hasa ya dharula ambayo hakuna mtu ambaye amepanga yatokee hasa hasa mafuriko,"alisema Mhandisi Kato.

Janga la Hanang lilitokea Desemba 3, mwaka jana mkoani Manyara na kusababisha vifo ya watu zaidi ya 80, huku mamia wengine wakiachwa bila makazi, uharibifu mkubwa wa miundombinu.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...