Na Mwandishi Wetu


KATIKA mazingira ya kupendeza ya Mkoa wa Geita, iko habari njema yenye kutia matumaini kwa waliokata tamaa na pengine kutengwa na jamii.

Shujaa wa habari hii ni Mgodi wa Dhahabu wa Geita, kampuni tanzu ya AngloGold Ashanti kwa kushirikiana na Kanisa Katoliki Jimbo la Geita na Baraza la Dhahabu duniani (WGC), wanaendesha mradi wa kusaidia watoto wenye ulemavu na kubadili mtazamo potofu wa jamii kuhusu ulemavu.

 Mradi huo wa ‘Ondoa imani potofu dhidi ya watoto wenye ulemavu’ wa miaka miwili wenye thamani ya dola za Marekani 99,200 unabadili maisha ya watu wenye ulemavu na kuacha alama chanya za kudumu kwa watoto wenye ulemavu na kufungua milango ya fursa kwao.

Kwa mudu mrefu sasa watoto wenye ulemavu mkoani Geita wamejikuta wakinaswa katika kilindi cha imani potofu kuhusu watu wenye ulemavu na huku jamii kubwa ikiamini kwamba ulemavu ni laana.

Kwa mujibu wa mratibu wa mradi huo, Joseph Massawe imani hizi zimesababisha watoto wanaozaliwa na ulemavu kunyanyapaliwa, kutengwa na wakati mwingine kutelekezwa na hivyo kusababisha watoto hao kukosa haki zao za msingi kama watoto na kama binadamu.

Hali hii ndiyo iliyosababisha GGML na Kanisa Katoliki kwa kushirikiana na Baraza la Dhahabu duniani kufikia uamuzi wa kuanzisha mradi huo ambao unalenga kutetea ustawi wa watoto na kuondoa dhana hiyo potofu kuanzia katika ngazi ya chini kwenye jamii pamoja na kutoa elimu ya uelewa kuhusu haki za watu wenye ulemavu katika nyanja za ksiasa, kijamii, kiuchumi na kitamaduni ili hatimaye kuondokana kabisa na dhana potofu kuhusu walemavu mkoani humo.

Akizungumzia namna mradi huo unavyotekelezwa, Massawe ambaye pia ni Mkurugenzi wa shughuli za afya wa Jimbo Katoliki la Geita, anasema walianza kwa kuzibainisha familia zenye watoto wenye ulemavu mbalimbali na kuanza kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuwapa fursa ya kutimiza ndoto zao kupitia vipaji walivyojaliwa.

“Kwanza tunabainisha familia zenye watoto wenye ulemavu, kisha tunaanza kutoa elimu ikiwa ni pamoja na kuwapeleka shule wale ambao wamefichwa nyumbani, na kuhakikisha wanalindwa dhidi ya aina yoyote ya ukatili ili hatimaye waweze kutimiza ndoto zao,” anasema na kuongeza kuwa malengo ya awali ni kuwafikia watoto wenye ulemavu 200 baada ya mwaka mmoja na kuhakikisha wanapewa mahitaji yao muhimu yatakayosaidia kukuza vipaji vyao katika elimu, michezo au shughuli zingine za kijamii.

“Kwa wale ambao tayari wapo shuleni na wale ambao tutawasaidia kujiunga na masomo tutawawezesha kupata mahitaji yao muhimu kwa kuzingatia aina ya ulemavu walionao,” anasema Massawe.

Ili kupanua wigo na kuufanya mradi huo kuwa endelevu wanakusudia kushirikiana na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali yanayosaidia watoto wenye ulemavu ili waweze kufikia ndoto zao kupitia elimu na kukuza vipaji mbalimbali.

 Mratibu huyo anasema mbali na mradi huo wa kuondoa mila potofu kwa jamii dhidi ya watu wenye ulemavu, Kanisa Katoliki Jimbo la Geita kupitia kituo cha Moyo wa Huruma pia wanatekeleza mradi wa kutunza watoto yatima ambao wazazi wao wamefariki kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.

Kituo cha Moyo wa Huruma kilianzishwa mwaka 2004, kupitia kampeni ya mgodi wa dhahabu wa Geita dhidi ya Ukimwi inayohusisha watu kupanda Mlima Kilimanjaro (Geita Gold Mine Kilimanjaro Challenge Against HIV/AIDS), Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Kanisa Katoliki Jimbo la Geita kimekuwa makazi ya watoto wenye uhitaji kuanzia mwaka 2006, malengo yake ya msingi yakiwa ni kuwalea watoto na kuwaandaa kuwa raia wema na wenye uwezo wa kujitegemea.

Kituo hicho tangu kuanzishwa kwake kimekuwa kikiendeshwa kwa ufadhili wa mgodi wa GGML na kwamba kuibuliwa kwa mradi wa kuondoa mila potofu dhidi ya watu wenye ulemavu ni mwendelezo wa mgodi huo kupanua wigo wa kushiriki shughuli za kijamii mkoani Geita na Tanzania kwa ujumla.

Matokeo ya mradi wa Ondoa Imani Potofu dhidi ya watoto wenye ulemavu yanajidhihirisha wazi katika Kituo cha Moyo wa Huruma, ambapo kimekuwa msaada mkubwa kwa watoto wenye ulemavu, kwa kuwa kinawawezesha kubadili maisha yao kwa kuwapa fursa mbalimbali za elimu, kuonesha na kukuza vipaji vyao.

Hapa watoto ambao pengine bila kupata fursa hiyo wasingeweza kudhihirisha uwezo na vipaji vyao. Kituo kimekuwa daraja muhimu la kuwavusha watoto ulemavu kutoka kwenye hali ya kuonekana kuwa tegemezi na kuwafanya kuwa sehemu muhimu ya jamii na kuwawezesha kutoa mchango wao kwa maendeleo yao na jamii wanamoishi kwa ujumla.

Mpango wa elimu kwa jamii hiyo dhidi ya unyanyapaa kwa watoto wenye ulemavu imekuwa ikihusisha kampeni kamambe ya kuvunja na kundoa kabisa mtazamo hasi kwa watu wenye ulemavu kwa kukabili ubaguzi wa tiba na kunyimwa haki kwa watu wenye ulemavu kupitia elimu, ambapo mradi unatoa elimu kwa jamii kwa kueleza uhalisia wa maumbile na sababu za ulemavu kisayansi ili kuondoa dhana potofu kwa baadhi ya wanajamii kwamba ulemavu unatokana na laana au makosa yaliyofanywa na wahusika au wazazi wao. Hii imelenga kubadili mtazamo wa jamii kuhusu ulemavu ili jamii iwapokee na kuwatendea kwa usawa bila ubaguzi.

Aidha, elimu hiyo inahusisha kuwaeleza jamii husika umuhimu wa kuwathamini na kuwapatia haki zao watoto wenye ulemavu kwa sababu wakipata fursa muhimu kama elimu na huduma za afya kwa usawa, wanao uwezo mkubwa wa kutoa mchango wao kupitia elimu na vipaji vyao kwa maendeleo ya jamii nzima.

Ukiondoa elimu kwa jamii, mkakati mwingine ni elimu kwa watoto wenye ulemavu ambao ndiyo hasa msingi wa mradi huu. Watoto wenye ulemavu wanapatiwa elimu katika ngazi mbalimbali, ambapo watoto wenye ulemavu wanapelekwa shule wameonesha na kudhihirisha kwamba walemavu wana mchango mkubwa kwa jamii wakipata usaidizi muafaka kadiri ya mahitaji yao.

Mbali na elimu ya msingi na sekondari; mradi pia unawapeleka watoto hawa kupata elimu ya ujuzi na stadi za kazi katika vyuo mbalimbali ili kuwawezesha kujitegemea ama kwa kuajiriwa au kujiajiri wenyewe kutokana na ujuzi wanaokuwa wamepata chuoni.

Huduma za afya ni shemu nyingine muhimu ya mradi, ambapo watoto wenye ulemavu mbali na kupelekwa shule na kuhudumiwa kwa mahitaji yao mengine, mradi unahakikisha kuwa wanapata haki ya matibabu pamoja na mahitaji kulingana na aina ya ulemavu kama fimbo kwa wasioona na vifaa vingine muhimu.

Hii inafanyika ili kwanza kuwapa haki sawa watu wenye ulemavu, lakini pia kama sehemu ya kupeleka ujumbe kwa jamii kwamba ulemavu siyo laana na wala ulemavu siyo kulemaa.

“Ni kweli mradi huu umefumbua macho watu wengi hasa kule vijijini ambako baadhi ya wazazi wamekuwa wakificha watoto wenye ulemavu bila kuwapeleka shule, wazazi wa aina hiyo wakija kuwakuta watoto wao kwenye kituo hiki na jinsi walivyobadilika wanakuwa mashahidi wa wenzao huko kwenye jamii, na hii inasaidia sana kubadili hisia na mtazamo potofu wa jamii kuhusu watoto wanaozaliwa na ulemavu,” anasema Masanja Malendeja mkazi wa Geita ambaye mtoto wa jirani yake aliyekuwa hajapelekwa shule aliokolewa na kituo hicho na sasa anaendelea na masomo kwa ufanisi.
Mkurugenzi wa shughuli za afya Jimbo Katoliki la Geita, Joseph Massawe.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...