SHIRIKA Lisilo la kiserikali la Karibu Tanzania Organisation (KTO,) limebeba ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia hususani gesi kupitia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 54 (FDC’s) vilivyopo nchini kote kwa kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na elimu pamoja ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kutunza mazingira na kuepukana na athari zitokanazo na matumizi ya nishati chafu ya kupikia ikiwemo vifo na magonjwa ikiwemo saratani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Mazingira, Mkurugenzi wa KTO Maggid Mjengwa amesema kuwa wamekutana na wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 54 vilivyopo katika Mikoa yote ya Tanzania kwa kuwa kila mmoja anaguswa na mabadiliko ya Tabia Nchi na vyuo hivyo ni miongoni mwa wananchi na vinapatikana wilayani na vijijiji na kupitia warsha hiyo mpango wa wananchi kutumia gesi safi ya kupikia na kuepukana na gesi chafu utafikiwa kwa kiasi kikubwa.

“Ajenda ya utunzaji wa mazingira ipo katika mpango mkakati wetu wa miaka mitano 2022/2027….Pia Rais wetu Samia Suluhu Hassan ameonesha njia na kuwa kinara katika kuhakikisha kila mtanzania anatumia nishati safi ya kupikia, Kupitia warsha hii iliyotukutanisha na wakuu wa vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi katika mikoa yote ni kuhakikisha jitihada na juhudi za Serikali inafanikiwa kwa kiasi kikubwa na ifikapo 2034 asilimia 80 ya watanzania iwe inatumia nishati safi ya kupikia.” Amesema.

Mjengwa amesema, katika warsha hiyo ya siku mbili wakuu hao wa vyuo 54 vya Maendeleo ya wananchi wamepitishwa katika mambo mbalimbali ikiweko Kampeni ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabia Nchi ikihusianishwa na afya ya uzazi.

“Katika vyuo hivi kuna Program ya Elimu Haina Mwisho ambayo hutolewa kwa mabinti waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito, wanapokelewa katika vyuo hivi na kusaidiwa ili wasiingie tena katika changamoto za afya za uzazi zilizowapata tunawafundisha ili wapate ujuzi na kufahamu masuala ya uzazi kwa ujumla.” Amesema.

Kuhusiana na kampeni ya mazingira amesema, Inakwenda sambamba na kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassani katika utunzaji wa mazingira na hiyo ni pamoja na kuendeleza kampeni ya kupanda miti katika vyuo vyote vya Maendeleo ya Wananchi na kuhakikisha kupitia vyuo hivyo wanatengeneza majiko bunifu yatayotumia nishati mbadala yatakayosaidia kutunza mazingira na kusaidia kundi la wanawake wanaozunguka vyuo hivyo wanaotumia muda mrefu kutafuta nishati za kupikia hususani kuni kuondokana na adha hiyo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dr. Erick Mgaya amesema, KTO ni mdau mkubwa kupitia vyuo hivyo ambavyo licha ya kutoa ujuzi vimekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya elimu, masuala ya jamii ikiwemo malezi na kuboresha maisha ya wananchi kupitia program mbalimbali ikiwemo Mpira Fursa na Elimu Haina Mwisho.

Amesema, kupitia vyuo hivyo wananchi wamebadilisha maisha yao kupitia program fupi na ndefu na kuwataka wananchi kutumia fursa zinazopatikana katika vyuo hivyo katika kuboresha hali za maisha pamoja na shughuli wanazozifanya.

Vilevile Dr. Adolf Luteyuga Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi amesema, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vilenge kutatua changamoto katika maeneo yao pamoja na kuboresha hali za maisha.

“Teknolojia inabadilika, Kupitia vyuo hivi wananchi wanafursa ya kuongeza ujuzi zaidi kupitia fani zao au kujiunga na vyuo hivyo ili kupata maarifa zaidi….Serikali inaunga jitihada za KTO kupitia vyuo hivi kwa kuhakikisha kunakuwa na mitaala pamoja na wakufunzi.” Ameeleza.

Kuhusiana na nishati safi ya kupikia Dr. Adolf Rutayuga amesema, wakuu wa vyuo 54 wamepata elimu kuhusiana na matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na athari za matumizi ya nishati chafu ya kupikia na kupitia wao elimu hiyo itafika katika Wilaya na Vijiji vyote nchini.

Awali Afisa Mchambuzi wa Idadi ya Watu na Maendeleo kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA,) Ramadhani Hangwa ameeleza kuwa katika warsha hiyo wametoa elimu juu ya masuala ya afya ya uzazi na mabadiliko ya Tabia Nchi.

“Tumeona kwamba Nchi yetu imeweza kupata neema ya mvua na makundi yote yanaathirika lakini wasichana na wanawake wamekuwa wahanga wakubwa wa mafuriko hayo na hali ya upatikanaji wa chanjo tumeona watumishi wa afya wakibeba mitungi ya gesi na chanjo katika mazingira magumu ya mafuriko hii inatupa ujumbe kwamba kuna umuhumu wa mipango yetu kujikita katika kuhakikisha miundombinu ya afya inapotengenezwa ihakikishe dawa na watoa huduma wawe wa kutosha katika nyakati zote za hali ya hewa.” Ameeleza.

Aidha amesema, Mipango inayopangwa katika ngazi ya msingi izingatie kuwa masuala ya afya ya uzazi yanakwenda sambamba na mabadiliko ya Tabia Nchi na kuangalia kwa umakini mahitaji ya makundi maalum ya wasichana, vijana pamoja na akina Mama kwa kuwa wao ni waathirika wakubwa wa mabadiliko ya Tabia Nchi.

Pia Monica Lukeha kutoka Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Sengerema mkoani Mwanza amesema kuwa Warsha hiyo iliyoaandaliwa na KTO na kuzinduliwa kwa kampeni ya mazingira pamoja na kupata elimu ya afya ya uzazi ni kampeni ambayo yenye tija kwa jamii na wameibeba kwa uzito wa hali ya juu.

Amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele suala la matumizi ya nishati safi ya kupikia na utunzaji wa mazingira na kupitia warsha hiyo wamepata uelewa zaidi na wataenda kutekeleza kwa vitendo kwa kuendelea kutumia nishati safi ya kupikia katika vyuo vyuo vyote ambavyo vinatumia nishati mbadala katika kuandaa chakula cha wanafunzi pamoja na kutunza mazingira kwa ujumla.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Ufundi Stadi Dr. Adolf Rutayuga akizungumza wakati wa Warsha hiyo na kueleza kuwa vyuo hivyo vilenge kutatua changamoto katika maeneo yao pamoja na kuboresha hali zao za maisha. Leo jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Sengerema Bi. Monica Lukeha akizungumza mara baada ya Warsha hiyo na kueleza kuwa wameibeba kampeni hiyo kwa uzito. Leo jijini Dar es Salaam.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...