Na Mwandishi wetu, Simanjiro

MAFURIKO yanayosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha yamekuwa kikwazo kwenye Kata ya Loiborsoit Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, baada ya kuingia kwenye makazi na mashamba.

Mafuriko hayo yameingia kwenye mashamba ya vijiji vya Loiborsoit B na Ngage, yamesababisha wakulima kutoendelea na shughuli za kilimo kutokana na maji kuongezeka maeneo ya umwagiliaji.

Diwani wa kata ya Loiborsoit, Siria Baraka Kiduya akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo amesema mafuriko hayo yameenea hadi maeneo ya makazi.

Amesema mafuriko hayo yamesababisha uharibifu wa miundombinu ya umwagiliaji na kushindikana kufanyiwa ukarabati.

“Kutokana na mafuriko kujirudia mara kwa mara ni vyema halmashauri ya wilaya kutupatia wataalam kupima matumizi bora ya ardhi ili kuokoa mifugo na mashamba vipindi vya ukame na mafuriko,” amesema Siria.

Amesema baadhi ya kaya zisizo na uwezo kuongezeka kutokana na athari ya hali ya hewa hivyo wanapaswa kuongezwa kwenye mfuko wa Tasaf kwani nao ni wahitaji.

Amesema ukosefu wa daraja la kuunganisha wilaya ya Simanjiro na Same mkoani Kilimanjaro, kunasababisha wagonjwa washindwe kusafarishwa kwenda hospitali kubwa na mifugo kutopelekwa mnadani.

“Tunapendekeza halmashauri ya wilaya ya Simanjiro kuwekeza kwa wakulima wa mpunga kupata mashine ya kuvunia (combiring harvester) na kupeleka mazao sehemu salama na kavu,” amesema Siria.

“Wananchi wanapaswa kupata mashamba ya nyanda za mvua ii kuepusha njaa na ukosefu wa mahitaji ya kila siku na wanafunzi kukosa chakula shuleni,” amesema Diwani huyo.

Amesema kijiji cha Loiborsoit B kimefanikiwa kujenga josho eneo la malisho na kuunda kamati ya usimamizi na kuratibu shughuli zote za josho.

“Zoezi la chanjo ya upele kwa ng’ombe limefanikiwa kwa asilimia 80 hivyo ugonjwa umedhibitiwa kwa chanjo ya lump skin vaccine na mifugo inaendela vizuri kiafya,” amesema Diwani huyo.

Amesema pia chanjo ya homa ya mapafu kwa mbuzi imefanyika kwa asilimia 70 na amewashauri wafugaji waendelee kujitokeza kwa ajili ya chanjo hiyo

Amesema baadhi ya wafugaji wa kata hiyo walijengewa uwezo kwa kupatiwa mafunzo ya ufugaji bora wa kisasa (SAIDA FAO) yalifanyika mjini Babati, Machi 28 mwaka 2024.

“Tunakabiliwa na baadhi ya changamoto ikiwemo dawa za ruzuku za kuogeshea mifugo hazijapatikana kwa muda wa mwaka sasa, vitambaa vya kuzuia ndorobo hakuna katika maeneo ya malisho,” amesema.

Amesema kuwekuwa na mbwa wengi vichaa mitaani ambao ni hatari kwa jamii ambao wametelekezwa pia hakuna eneo la machijio katika kitongoji cha Ngage B na kusababisha ukaguzi wa nyama kuwa mgumu.


"Pia nimeomba vyandarua na kuitaji maeneo ya vitongoji ya Ndepes Jangwani na Mazinde kupatiwa maji safi na soko jana tumeazimia kuwanzishwa mnada kijiji cha Ngage," amesema.

“Tunashauri ombi la majosho katika eneo la kitongoji cha Mazinde kijiji cha Loiborsoit B, Ngage A, Songoyo, tunaomba wenyeviti wa vijiji na vitongoji waendelee kuhamasisha wafugaji waweze kufikia ufanisi mkubwa wa kuchanja mifugo,” amesema.

Amesema shule zote nne za msingi na moja ya sekondari ya kata ya Loiborsoit wanafunzi wote wanapata chakula cha mchana, bado wanaendelea kuhamasisha wazazi na walezi kupeleka chakula shuleni.

Amesema kwenye matokeo ya kidato cha pili katika shule ya sekondari Loiborsoit kwa mwaka 2023 ufaulu ulikuwa kwa asilimia 100.

Amesema kwa upande wa kuripoti kwa wanafunzi wa madarasa ya awali na la kwanza kwa mwaka 2023/2024 umefanyika kwa asilimia 100.

“Mikakati ya kitaaluma iliyopo ni kufanya majaribio na mazoezi na mitihani ya upimaji, kufundisha kwa muda wa ziada na ufundishaji wa siku zisizo za masomo,” amesema.

Amesema walimu wamejipanga kumaliza silabasi kwa wakati na kufanya marudio na kuwepo kwa mitihani ya majaribio yenye hadhi kwa lengo la kufanya watambue maswali yanayotokana na mitihani ya taifa.

Amesema wamelenga kudhibiti utoro wa rejareja kwa wanafunzi kwa kuwaandikia barua wazazi, walezi na viongozi wa vijiji na kata.

Amesema shule shikizi ya Ngage A imefikia kwenye lenta, michango ya wananchi 1,000,000 shule shikizi ya Songoyo vifaa vipo eneo la ujenzi, mawe, mchanga na kokoto na michango ya shilingi 590,000.

Kata ya Loiborsoit ina vijiji viwili vya Ngage na Loiborsoit B, ambapo kijiji cha Ngage kina vitongoji vya Ngage A, Ngage B na Ndepes na kijiji cha Loiborsoit B ina vitongoji vya Engurush, Oltibu na Mazinde.

Kata ya Loiborsoit upande wa kaskazini imepakana na kata ya Ngorika, kusini kata ya Ruvu Remit, magharibi kata ya Endonyongijape na kata ya Langai na mashariki mto Pangani.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...