Vifaa Tiba vyenye thamani ya zaidi ya Mil. 28 vimetolewa na Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini Mhe. Abdulaaziz M. Abood kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma za Afya ili kupunguza na kuondoa kabisa changamoto ya kukosa baadhi ya vipimo kwenye Zahanati husika wakati wa kutoa huduma hiyo kwa wananchi kwa sababu tu ya kukosekana Mashine za vipimo vya baadhi ya magonjwa yanayowasumbua wananchi.

Mbunge huyo ametoa Vifaa Tiba hivyo katika Kata tano zilizopo kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mey 8 Mwaka huu wakati wa ziara yake ya kutembelea na kukagua maendeleo ya Zahanati ya Mbete na Towero zilipo kata ya Mlimani, Zahanati ya Kibwe Kata ya Boma, Zahanati ya Uwanja wa Taifa iliyopo Kata ya Uwanja wa Taifa, Zahanati ya Konga iliyopo Kata ya Mzinga pamoja na Kituo cha Afya cha Sina kilichopo Kata ya Mafisa.

Vifaa vilivyotolewa kwenye ziara hiyo ni pamoja na Vitanda vya huduma ya kwanza vitatu (3), Vitanda vya kusaidia Kinamama wajawazito kujifungua (Derivery Bed) 3, Hadubini (Microscope Tube) 4, Sentrifyugi Mashine 5 pamoja na Mashine maalum ya kumsaidia mgonjwa kupumua haswa Kinamama wajawazito, Mashine 1 na Vifaa vinginevyo kama vile Glucose Mashine 5, ambavyo kwa ujumla wake vifaa hivyo vimegharimu kiasi cha zaidi ya Tsh. Mil. 28 zilizotoka mfukoni mwa Mbunge huyo ili kurahisisha na kuboresha huduma za Afya kwa wananchi wa Jimbo hilo.

Aidha, Mbunge huyo amebainisha kuwa, lengo kuu la kupeleka Vifaa hivyo ni kutaka kuona wananchi wa Jimbo hilo wanapata huduma faafu za Kiafya ili wawe chachu ya kulijenga Taifa la Tanzania, hivyo amewataka wataalamu wa Afya kuvitumia kikamilifu kwa kuleta matokeo chanya, ambapo amewarai wananchi katika maeneo tofauti kutumia Zahanati hizo pamoja na vituo vya Afya vya Serikali ili kuonesha kuwa uwekezaji huo wa Vifaa unakuwa na tija kwenye utoaji wa huduma za Afya ndani ya Jimbo hilo.

“Lengo la kununua na kuleta vifaa hivi ni kuona namna ya kuboresha huduma za Afya katika Manispaa yetu kwa kuona wananchi wanahudumiwa kikamilifu, vile vipimo ambavyo awali havikupatikana Kwenye Zahanati husika, sasa vipatikane na wananchi wahudumiwe………..

…….. nitoe rai kwenu wananchi, sasa anzeni kutumia Zahanati zenu na Vituo vya Afya vya karibu yenu na vilivyo vya Serikali ili kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutoa fedha na kuboresha huduma zetu za Afya na tuache kuhangaika.” Amebainisha Mbunge Abood.

Katika hatua nyingine, Mbunge huyo ametimiza ahadi ya Mifuko 45 ya saruji katika Mitaa ya Kikundi, Kisosa na Chalagule na Chepe 5 katika Kata ya Mlimani kufuatia maombi ya wananchi wa Kata hiyo wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika Februari 29 Mwaka huu, ambapo Mbunge aliahidi kusaidia vifaa hivyo ili kurekebisha na kujenga Vivuko katika Mitaa tajwa na kuwezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za uzalishaji mali.

Kwa upande wake ndugu Muhammed Thabiti ambaye ni Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Boma, kwa niaba ya Makatibu na Wenyeviti wa Chama hicho wa Kata zilizofikiwa na Vifaa hivyo, amemshukuru Mbunge wa Jimbo hilo kwa Msaada huo kwani, unaenda kufanya maboresho katika huduma za Afya kwenye Kata husika. 

Katibu huyo kupitia shukrani zake ameongeza kuwa, Mbunge Abood ni Mbunge wa mfano, mtatuzi wa shida za wananchi kwa wakati, hupatikana wakati wote na hutekeleza kwa vitendo ahadi anazozitoa, kwani ni muda mchache tu tangu afanye ziara katika Kata hizo na sasa ameweza kutekeleza.

Naye Diwani wa Kata ya Mlimani iliyopo katika Jimbo hilo Mhe. Zinduna Kombo kupitia Chama tawala, akiwakilisha Madiwani wanufaika wa mradi amesema kwamba Chama tawala kinatekeleza Ilani kwa vitendo kuanzia kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusogeza huduma za Afya kwa wananchi kwa kujenga Hospitali, Vituo vya Afya pamoja na Zahanati, ambapo kwa upande wa Jimbo la Morogoro Mjini Mhe. Abood ameamua kujitoa ili kusaidia vifaa tiba kwa lengo la kuunga Mkono jitihada za Rais.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...