Na Mwandishi Wetu

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umetoa mafunzo ya Usalama na Afya kazini kwa wabunge chini ya Umoja wa Wabunge Vijana Tanzania (TYPF) 100, ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa Taasisi hiyo kuhakikisha makundi mbali mbali katika jamii yanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu kanuni bora za usalama na afya mahali pa kazi.

Mafunzo hayo ambayo yamefanyika katika ukumbi wa OSHA Jijini Dodoma yalifunguliwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi, ambaye alimwakilisha Waziri wake, Deogratius Ndejembi.

Akifungua mafunzo hayo, Naibu Waziri Katambi amesema OSHA inaowajibu mkubwa wa kulinda nguvukazi ya Taifa hususan vijana ambao ndio wanaunda asilimia kubwa ya nguvukazi inayotumika katika uzalishaji nchini na duniani kote.

“Kazi kubwa ya serikali kupitia OSHA ni kuwalinda wafanyakazi ili wasipate ajali, magonjwa au vifo vitokanavyo na kazi kwani kunapokuwa na wagonjwa wengi manake Serikali inapata mzigo mkubwa wa kuwahudumia na hivyo kuathiri uchumi wa nchi kutokana na fedha nyingi kutumika kununua madawa na vifaa tiba pamoja na uzalishaji kushuka kutokana na nguvukazi kupungua na muda wa uzalishaji kupotea kwa kuuguza wagonjwa,” amesema Naibu Waziri Katambi.

Katambi amewashauri wabunge hao waliopatiwa mafunzo kusaidia kusambaza elimu juu ya umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usalama na afya nchini ili kuwalinda vijana na wananchi wote kwa ujumla dhidi ya vihatarishi vya ajali na magonjwa katika shughuli mbali mbali za uzalishaji.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Vijana Tanzania (TYPF) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulika Elimu, Zainab Katimba, amesema lengo la semina hiyo ilikuwa ni kuwajengea uelewa wabunge vijana katika eneo la usalama na afya mahali pa kazi.

“Kupitia mafunzo haya tumejifunza mengi hususan dhana ya vihatarishi katika maeneo yetu ya kazi na tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa. Hivyo, tutakuwa katika nafasi nzuri zaidi kuendelea kuishauri serikali pamoja na kuwashirikisha elimu hii wananchi wetu,” ameeleza Bi Katimba.

Washiriki wengine wa semina hiyo akiwemo Ng’wasi Kamani, Mbunge wa Vijana Taifa Pamoja na Venant Daud, Mbunge wa Jimbo la Igalula wameeleza umuhimu wa mafunzo hayo kwao na wananchi wanaowaongoza.

“Mafunzo haya tuliyoyapata ni muhimu sana kwetu sisi kama wabunge vijana ambao tunao wajibu wa kusaidia kuwaelimisha vijana wenzetu na wananchi kwa ujumla,” ameeleza Mbunge Venant Daud.

“Sisi ni wawakilishi wa wananchi wakiwemo wafanyakazi serikalini na sekta binafsi, usalama wao ni kitu cha msingi sana na hapo ndipo OSHA inapoingia. Kwahiyo yale tuliyojifunza na yale tunayoyaona OSHA ikiyasimamia ndio yanapelekea kuuona utulivu uliopo katika shughuli za uzalishaji nchini,” amesema Ng’wasi Kamani.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema mafunzo hayo ni mwendelezo wa mkakati wa Taasisi ya OSHA kuyafikia makundi mbali mbali nchini na kuyajengea uelewa wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.

Amesisitiza kwamba mafunzo ya usalama na afya ni muhimu kwa wafanyakazi wote nchini hususan vijana ambao ndio washiriki wakubwa katika shughuli za uzalishaji ambapo tafiti mbali mbali ukiwemo utafiti uliofanywa na OSHA mwaka 2022 zinaonesha kwamba vijana ndio wanaoathirika zaidi na ajali na magonjwa mahali pa kazi.

Naibu Waziri - Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi akifungua Mafunzo ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi kwa Wajumbe wa Jumuiya ya Umoja wa Wabunge Vijana Tanzania yaliyo andaliwa na OSHA Jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda akitoa wasilisho kwa Wajumbe wa Jumuiya ya Umoja wa Wabunge Vijana Tanzania juu ya majukumu, wajibu na mwenendo wa Taasisi ya OSHA wakati wa Semina ya Mafunzo ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi kwa Wabunge hao iliyofanyika katika Ofisi za OSHA Jijini Dodoma.

Afisa Mafunzo wa OSHA, Bw. Simon Lwaho akiwasilisha mada juu ya namna ya kutambua na kudhibiti aina mbalimbali za vihatarishi vya maeneo ya kazi kwa Wajumbe wa Jumuiya ya Umoja wa Wabunge Vijana Tanzania wakati wa Semina emina ya Mafunzo ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi kwa Wabunge hao.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda akizungumza na Wanahabari wa Mkoani Dodoma wakati wa Semina maalumu ya uelewa wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi iliyoandaliwa na OSHA kwa lengo la kuwarahisishia utoaji taarifa zinazohusu masuala ya usalama na afya kadhalika shughuli mbalimbali za zinazofanywa na OSHA.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...