Na Mwandishi wetu,Tunduru

WAKALA wa barabara (TANROADS)Mkoa wa Ruvuma,umepokea Sh.bilioni 2.5 kati ya Sh.bilioni 6 ilizoomba ili kurejesha miundombinu ya barabara zilizoharibiwa na mvua za masika katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Hayo yamesemwa jana na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Saleh Juma,baada ya kukagua kazi ya urejeshaji wa miundombinu ya daraja la Mto maarufu la Namiungo wilayani Tunduru.

Saleh,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan,kwa kuidhinisha fedha hizo ambazo zitatumika kwa ajili ya matengenezo ya barabara kwenye maeneo yenye changamoto ili kutoa fursa kwa shughuli za usafiri na usafirishaji kuendelea kama kawaida.

Aidha alisema,licha ya mvua za masika kunyesha kwa wingi mkoa Ruvuma,lakini barabara zote zilizo chini ya TANROADS zinapitika na hakuna shughuli za kijamii zilizosimama kutokana na ubovu wa barabara.

Alisema,mwezi Machi mwaka huu daraja la Namiungo lilipata athari kubwa baada ya maji ya mvua kupita juu ya daraja na kuharibu miundombinu,hali iliyosababisha magari kupita upande mmoja.

Alisema,kazi ya kurejesha miundombinu ya daraja hilo imechelewa kukamilika kutokana na changamoto ya mvua, ambapo magari ya mkandarasi yameshindwa kufika maeneo yanakopatikana mawe na vifusi.

Hata hivyo,amemtaka mkandarasi kuhakikisha anakamilisha kazi mwishoni mwa mwezi huu ili barabara hiyo irudi kwenye hali yake na wananchi waendelee kuitumia katika shughuli zao za uzalishaji mali.

“tunamshukuru mkandarasi kwa kazi kubwa aliyofanya hadi sasa,hata hivyo tunataka aongeze kasi ili kazi zote zilizopangwa zikamilike ifikapo mwishoni mwa mwezi huu, kwa sasa hivi hali ya hewa ni nzuri na hakuna changamoto yoyote”alisema Saleh.

Mhandisi wa kampuni ya Ovans Constructions Ltd iliyopewa kazi ya matengenezo ya daraja la Namiungo Azimio Mwapongo alisema,wameshindwa kukamilisha kazi kwa muda uliopangwa kutokana na mvua ambapo magari yalishindwa kufika kwenye maeneo yanapopatikana mawe na udongo.

Amehaidi kufanya kazi usiku na mchana ili waweze kukamilisha kazi mwisho wa mwezi huu na ameishukuru ofisi ya meneja wa Wakala wa barabara TANROADS mkoa wa Ruvuma kwa ushirikiano unaowapa.

Mkazi wa kijiji cha Namiungo Juma Daud,ameipongeza serikali kwa kuharakisha urejeshaji wa miundombinu katika daraja hilo kwani litawezesha watumiaji wake hasa wenye magari makubwa na madogo kupitia bila wasiwasi.

Ameishukuru TANROADS, kuwapa kipaumbele cha kazi wakazi wa kijiji hicho ambao wanaendelea kunufaika na miradi ya ujenzi wa barabara pindi inapotokea changamoto ya uharibifu wa miundombinu kwenye barabara kuu ya Songea-Mangaka.
Mhandisi wa kampuni ya Ovans Constructions Ltd Azimio Mwapongo kulia,akimsikiliza Meneja wa TANROADS Mkoani Ruvuma Mhandisi Saleh Juma aliyefika katika daraja la Namiungo kwa ajili ya kukagua kazi ya ukarabati wa daraja hilo ambalo kingo zake ziliharibika baada ya kusombwa na maji.

Meneja wa TANROADS Mkoani Ruvuma Mhandisi Saleh Juma,akikagua kazi ya ukarabati wa miundombinu ya daraja la Namiungo wilayani Tunduru lililoathirika na mvua za masika baada ya maji kusomba upande mmoja wa daraja hilo,kulia ni mkuu wa kitengo cha mipango TANROADS Mhandisi Rubara Marando na katikati Mhandisi wa kampuni ya Ovans Constructions Ltd inayofanya ukarabati huo Azimio Mwapongo.

Mafundi wa kampuni ya Ovans Constructions Ltd wakiendelea na ukarabati wa miundombinu katika daraja la Namiungo wilayani Tunduru lililoharibika baada ya kingo za daraja hilo kusombwa na maji ya mvua za masika mwezi Machi mwaka huu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...