Serikali imesema hadi sasa watumishi wa umma 25,039 wamehamia Makao Makuu ya Nchi Jijini Dodoma pamoja na  Taasisi  65 ambapo inaendelea na  mpango kazi wa  ujenzi wa Awamu ya Pili wa majengo ya Ofisi za Wizara na Taasisi unaotarajiwa kukamilika  mwaka 2025.

Hayo yalisemwa leo tarehe 21 Mei, 2024 Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri  Ofisi ya Waziri Mkuu  anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Mhe.  Ummy Nderiananga wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Bahi, Mhe. Keneth Nollo aliyehoji ni lini mpango wa  kuhamia Dodoma utakamilika na ni taasisi ngapi zimeshahamia mpaka sasa.

Mhe. Nderiananga alieleza kwamba Mpango wa kuhamisha Makao Makuu ya Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda  Dodoma ulianza rasmi mwaka 2016.

“Hadi sasa, jumla ya watumishi 25,039 kutoka Serikali kuu, Bunge, Mahakama, Vyombo vya Ulinzi na Usalama, pamoja na Taasisi 65 wameshahamia  na wanaendelea kutekeleza majukumu yao wakiwa Dodoma. Pia Serikali  inatarajia kukamilisha mpango wake wa kuhamia Dodoma kwa kuzingatia Mpango kazi Maalum wa ujenzi wa Awamu ya Pili ya ujenzi wa ofisi hizo,”Alisema Mhe. Nderiananga.

Kuhusu ujenzi wa nyumba za watumishi alibainisha kuwa Serikali ilianza ujenzi wa makazi rasmi ya viongozi  kuanzia mwaka  2021/2022 kupitia Wakala wa Majengo  Tanzania (TBA) ambapo nyumba 20 zilijengwa wakati hadi kufikia  Mwezi Septemba mwaka 2023 nyumba za watumishi  150 ikiwemo nyumba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kwa sasa tuko kwenye zoezi la kupanga eneo ambalo tumelitoa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za viongozi  wa Serikali na watumishi wa umma  tutakuwa na Ekari 4654 kati ya Mji wa Serikali Mtumba na Ikulu,”Alieleza Mhe. Nderiananga.

Aidha, aliwahakikishia Watanzania kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea  na mpango wake wa kuendeleza Mji wa Serikali- Mtumba kama ilivyokusudiwa.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...