Na Pamela Mollel,Arusha

Zaidi ya washiriki 700 kutoka mashirika ya umma, sekta za fedha na ukaguzi wa mahesabu nchini wamekutana Arusha kujadili faida na changamoto zinazotokana na maendeleo ya teknolojia mpya za kidijitali.

Mkurugenzi Mtendaji wa bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), Pius Maneno amesema ingawa huu ni moja ya mikutano yao ya kawaida ya kila mwaka lakini vikao vya mwaka huu ni maalumu katika kujadili masuala ya kidijitali.

Mkutano huu wa 15 unawashirikisha Wahasibu, Wakaguzi wa Hesabu, Wakufunzi na Watendaji wa benki uliondaliwa na bodi ya wahasabu na wakaguzi wa hesabu (NBAA) na Benki Kuu ya Tanzania.

“Tunajadili majukumu yetu katika utendaji Mabadiliko ya Kidijitali katika utoaji wa huduma za kifedha na taarifa za fedha pamoja na ulinzi pamoja na usalama wa taarifa hizo dhidi ya udukuzi, au Cybersecurity,” alisema Mkurugenzi huyo wa NBAA.

Amesema kuwa wanaongelea suala la Masoko ya hisa na jinsi yanavyoweza kutumia taarifa za kidijitali, ili kuendeleza ufanisi katika utendaji ili kupata matokeo mazuri katika masoko ya mitaji pamoja na jinsi usajili wa makampuni unavyoweza kuboroshwa kidijitali.

Mmoja wa washiriki wa mkutano huu wa siku tatu, Sarah Malay ambaye ni mfanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania anasema kuwa wameanza kujifunza masuala mengi kuhusu maendeleo ya kidijitali, ikiwemo kudhibiti utakatishaji fedha, na mihamala haramu.

Mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano huo ambaye ni Naibu Gavana wa Benki kuu ya Tanzania Daktari Yamungu Kayandabila alisema kuwa maendeleo ya teknolojia ya kidijitali katika utoaji wa taarifa yanasaidia kupunguza matumizi ya machapisho ya kwenye makaratasi.

“Na pia kwa sasa sio lazima kuwa na majengo mengi ya ofisi maana mawasiliano na uchakataji wa taarifa unaweza kufanyika popote kutokana na maendelo ya kidijitali, hivyo gharama nyingi zimeweza kuokolewa,” alisema Dk Kayanyabila na kuongeza kuwa hii pia husaidia katika kupunguza athari za uchafuzi wa mazingira.

Hata hivyo naibu Gavana huyo aliongeza kuwa pamoja na faida husika lakini safari ya kuelekea katika maendeleo ya teknolojia ya kidijitali pia ina changamoto zake zikiwemo zile za gharama za miundombinu, udukuzi wa taarifa na suala la watu wengi kuwa nje ya mfumo husika.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...