Na Mwandishi Wetu -WKS

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema kuwa ni vyema Wizara ya Katiba na Sheria kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ikaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu faida za kufanya usuluhishi wa migogoro nje ya Mahakama ili kuepuka kutumia muda mrefu kusikiliza Mashauri, kuepuka gharama kwa wanaohusika katika migogoro (Wadaawa) na kuepuka msongamano wa Mashauri Mahakamani.


Profesa Ibrahim alisema hayo katika mazungumzo na Naibu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini wakati alipomtembelea Jaji Mkuu katika Ofisi za Mahakama ya Rufani Kivukoni Jijini Dar es Salaam Juni 20,2024 kwa lengo la kufahamu majukumu na muundo wa Muhimili wa Mahakama, Kuimarisha mashirikiano baina ya Wizara na Muhimili na kujifunza namna walivyoweza kufanikiwa kwenye masuala ya miradi ya maendeleo na matumizi ya TEHAMA.


“Katiba ya Tanzania katika kipengele cha utoaji haki, inasisitiza katika kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya wanaohusika katika migogoro. Suala la kusuluhishwa kwa dakika thelathini linaweza kuchukua miaka zaidi ya kumi. Zipo baadhi ya Nchi ambazo zaidi ya asilimia tisini na tano (95%) ya Mashauri yanaisha kwa njia ya Usuluhishi. Ni vyema Sheria ielekeze kuwa, kabla ya suala kwenda Mahakamani lianze kwenye Usuluhishi kwani najenga ukaribi na sio uadui.” Alisema Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma.


Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini ameupongeza Muhimili wa Mahakama kwa kazi kubwa wanazofanya katika kusimamia utoaji haki kwa Wananchi, kusimamia ujenzi wa Mahakama katika maeneo mbalimbali Nchini na pia kufanya mageuzi katika utendaji wa Mahakama ikienda sambamba na matumizi ya TEHAMA.


Katika mazungumzo hayo, Naibu Waziri Sagini amesema katika kipindi cha nyuma cha utendaji kazi kama Katibu Tawala, kumekuwa na changamoto ya Kamati ya Maadili ya Mahakimu katika ngazi za Wilaya na Mikoa kutokutana na kufanya vikao na limekuwa likisahaulika ambapo Jaji Mkuu amesema kuwa kwa sasa Kamati hiyo ikiwa na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama imekuwa ikizunguka katika Mikoa mbalimbali Nchini kwa lengo la kuzijulisha Kamati za Wilaya na Mikoa namna ambavyo zinatakiwa kufanya kazi na kuzijengea uwezo zaidi.


Kikao hicho kilihudhuriwa na Msajili Mkuu wa Mahakama Mhe. Eva Kiaki Nkya, Msajili wa Mahakama ya Rufani Mhe. George Hillary Herbet, Naibu Msajili Mahakama Kuu Mhe. Venance Mlingi ambaye pia ni Katibu wa Jaji Mkuu wa Tanzania na Mhe. Hakimu Mkazi Jovine Constatine ambaye pia ni Katibu wa Msajili Mkuu wa Mahakama.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...