Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema kuwa Kampuni ya Volt Graphite Tanzania Limited (VGT) ipo katika majadiliano ya mwisho na wanunuzi wa Madini ya Kinywe (Graphite) ili kuruhusu kuanza kwa ujenzi wa kiwanda cha kuongeza thamani ya madini hayo Wilayani Masasi, Mkoa wa Mtwara.

Ameyasema hayo leo Juni 07, 2024, Bungeni, Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Ndanda Mhe. Cecil Mwambe aliyetaka kujua kuhusu mpango wa Serikali kuhakikisha uchimbaji wa madini ya Kinywe unatekelezwa katika Kata ya Chiwata, Wilayani Masasi.

Akijibu, Dkt. Kiruswa amesema kuwa, Wizara ya Madini ilitoa leseni mbili za Uchimbaji wa Kati zenye namba ML 591/2018 na ML 592/2018 kwa Kampuni ya Volt Graphite Tanzania Public Limited ili kuendesha shughuli za uchimbaji wa madini ya kinywe katika mradi wa Mbunyu, Ndanda.

Amesema, hata hivyo, uchimbaji huo haujaanza tangu leseni hizo kutolewa kutokana na kuchelewa kwa makubaliano kati ya VGT na wanunuzi wa madini hayo.

Naibu Waziri Kiruswa ameongeza kuwa, kwa sasa, mwekezaji amesaini mkataba na Kampuni ya Property Matrix Limited (PML) kwa ajili ya kufanya tathmini ya ulipaji fidia kwa wananchi waliopo kwenye eneo la mradi. Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha fidia stahiki inatolewa kwa wakazi ambao watapitiwa na mradi huo.

“Aidha, Kampuni ya Volt Graphite Tanzania ipo katika majadiliano ya mwisho na wanunuzi wa madini ya kinywe ili kuruhusu kuanza kwa ujenzi wa kiwanda cha kuongeza thamani ya madini hayo” amesema Dkt. Kiruswa.

Dkt. Kiruswa amesisitiza kuwa, Mradi wa Mbunyu utakapoanza kutekelezwa unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa wakazi wa Kata ya Chiwata na Jimbo la Ndanda kwa ujumla kupitia ajira, maendeleo ya kiuchumi, na kuimarisha miundombinu katika eneo hilo.

Ametoa wito kwa wanaozunguka mradi huo kuchangamkia fursa za kutoa huduma katika mradi huo pindi shughuli za uchimbaji zitakapoanza baada ya kukamilika kwa majadiliano na taratibu zote zinazohitajika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...