* picha za mabondia kuwekwa katika kuta za ubalozi wa Ufaransa nchini na Houlgate, Normandy na Paris nchini Ufaransa
Na Leandra Gabriel, Dar es Salaam
SERIKALI Ya Ufaransa kupitia Ubalozi wake nchini imeeleza kuwa suala la ushiriki wanawake katika michezo na kuendeleza vipaji ni moja ya kipaumbele chao na hiyo ni pamoja na kuhakikisha wanawake wanashiriki katika michezo mbalimbali ukiwemo mchezo wa Boxing, ambapo Ubalozi huo kwa kushirikiana na kituo cha utamaduni cha ubalozi ’Alliance Francaise’ wamezindua mradi wa ‘Boxing Queen’ mahususi kwa kuwainua wanawake wanaocheza mchezo huo.
Akizungumza leo katika ofisi za Ubalozi huo jijini Dar es Salaam, Balozi wa Ufaransa nchini Nabil Hajlaoui amesema, mchezo wa ngumi nchini Tanzania umekuwa ukiendelea kukua na kufanya vizuri licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazowakumba wanawake katika mchezo huo.
“Idadi kubwa ya wanawake wanajihusisha na mchezo wa ngumi maarufu kama Boxing’ katika kutimiza malengo yao, kupitia mradi huu wa Boxing Queens utawasaidia kwa kiasi kikubwa wanawake wa kitanzania kutimiza ndoto zao kupitia Boxing kimataifa.” Amesema.
Balozi Nabil amesema, kupitia mradi huo picha za mabondia hao zitaonekana katika kuta za ubalozi huo hapa nchini pamoja na maeneo yenye vivutio zaidi nchini Ufaransa ambako pia dunia itatazama huko kupitia maonesho makubwa duniani ya Olympic yatakayozinduliwa Julai, 26 mwaka huu.
“Mradi huu ni muunganiko wa ubunifu na michezo na ni sehemu ya kuendeleza kundi hili ambalo Rais Samia alipofanya ziara nchini Ufaransa na kuzindua mkakati wa nishati safi ya kupikia na mwenyeji wake Rais Macron alieleza umuhimu wa kuendeleza kundi la vijana na wanawake kwa kuzingatia usawa na kuboresha hali zao za maisha.” Ameeleza.
Aidha amesema, Delphine Blast ambaye ni msimamizi wa mradi huo kwa siku kadhaa amekuwa akiwafuatilia mabondia hao wakati wa mazoezi, kufuatilia maisha yao ya kila siku pamoja na mapambano wanayoshiriki ili kufahamu changamoto wanazokabiliana nao
Kwa upande wake mpiga picha wa kimataifa na muasisi za mradi huo Delphine Blast amesema, fani ya ngumi inakua kwa kasi na wanawake wanaoshiriki mchezo huo wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo vifaa vya mazoezi, fedha pamoja na jamii kutoamini katika mchezo huo.
Amesema alianza mradi wa Queen Boxing mwaka 2023 jijini Arusha kwa lengo la kufahamu wanachopitia mabondia hao ndani na nje ya ulingo na kuyaleta kwa jamii ili waweze kupata ushirikiano na kutimiza ndoto zao kupitia mchezo huo.
Ameeleza kuwa licha ya wanawake hao kushiriki katika mchezo huo kwa kupigana ulingoni pia wanapigania haki na uhuru wao hivyo wanastahili kupewa ushirikiano ili waweze kutimiza malengo na kupitia Picha hizo zitakazowekwa katika kuta za ubalozi na maeneo mbalimbali nchini Ufaransa zitatoa fursa zaidi katika kufikia malengo yao na kuhamasisha wanawake wengi zaidi kushiriki mchezo huo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya wanawake ya Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania Bi. Asha George amesema kuwa hiyo ni fursa kubwa kwa mabondia wa kike nchini katika kukuza vipaji vyao kimataifa.
Ameushukuru ubalozi wa Ufaransa kwa kuendeleza ushirikiano mzuri na Tanzania ambapo kupitia mradi wa Queen Boxing changamoto za mabondia kutoonekana kutokana na kukosa fursa, vifaa duni na kukosa fursa za kushiriki mashindano ya kimataifa zitajibiwa na kuwataka mabondia hao kuzingatia maadili na kuwa na nidhamu ili waweze kutimiza ndoto zao.
Pia amesema mradi huo utainua wanawake wengi zaidi katika mchezo huo na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta chachu katika sekta ya michezo ambapo kwa mara ya kwanza wameleta medali ya fedha nchini kupitia mashindano ya wanawake Afrika pamoja na kupata fursa ya kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Baadhi ya mabondia wakiwemo Pendo Njau, Halima Bandola na Leyla Macho wameeleza kufurahishwa na fursa hiyo itakayowatambulisha kimataifa na kuiomba Serikali kuendeleza michezo ya namna hiyo hususani kwa wanawake.
Katika suala la michezo na usawa katika sekta hiyo tayari Ubalozi huo umefanya kazi na taasisi mbalimbali ikiwemo Women Empowerment Zanzibar (WEZA,) na kufanikisha kuipelekea timu ya wanawake katika mashindano ya mpira wa miguu Mei, 2024 Brittany, Ufaransa na hiyo ni pamoja na kutoa elimu ya masuala ya afya ya uzazi, uboreshaji wa maeneo ya mazoezi pamoja na vifaa. Balozi wa Ufaransa Nchini Tanzania Nabil Hajloui akizungumza wakati wa hafla hiyo na kueleza kuwa uendelezaji wa michezo ni moja ya kipaumbele chap hususani kwa kundi la wanawake kwa kuhakikisha wanainuka na kufikia malengo yao. Leo jijini Dar es Salaam.
Muasisi wa mradi wa Queen Boxing Delphine Blast akizungumza wakati wa hafla hiyo na kueleza kuwa ameshiriki kushuhudia maisha ya mabondia hao ndani na nje ya ulingo na kuyaleta kwa jamii ili iweze kushiriki katika kufanikisha ndoto zao. Leo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake ya Shirikisho ya Ngumi za Ridhaa Tanzania Asha George akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya hafla hiyo na kuwataka mabondia hao kuwa na nidhamu ili waweze kunufaika na miradi ya aina hiyo. Leo jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Ufaransa nchini Nabil Hajloui (kushoto,) akiteta jambo na Balozi wa Marekani nchini Michael Battle (kulia,)Leo jijini Dar es Salaam.
Matukio mbalimbali wakati wa hafla hiyo.
Baadhi ya mabondia wakizungumza na waandishi wa habari na kueleza kufurahishwa na mradi huo utakaowatambulisha kimataifa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...