
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka wahitimu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kuzingatia maadili, miongozo na kuheshimu mipaka ya kazi yao ikiwemo utunzaji wa siri ambazo watazifahamu katika utendaji kazi wao.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati aliposhiriki Mahafali ya 39 ya Chuo
cha Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Amesema kushindwa kutunza siri za Serikali kunadhoofisha ufanisi na kurudisha nyuma hatua za utekelezaji wa majukumu mbalimbali na wakati mwingine hupelekea uhasama kati ya
watumishi na kuvuruga utendaji kazi na uhusiano mwema kazini.
Amesema kwa sasa Utumishi wa umma unakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha na mali ya umma, matumizi mabaya ya ofisi za umma, kutowajibika na mmomonyoko wa maadili.
Vilevile Makamu wa Rais ametoa wito kwa Waajiri wote nchini kuzingatia maelekezo ya Waraka wa Utumishi wa Umma Namba 5 wa mwaka 2011 unaowataka waajiri katika Utumishi wa Umma kutenga fedha ili kuhakikisha watumishi wapya wote wanapatiwa mafunzo elekezi ya awali ndani ya kipindi
cha miezi mitatu mara baada ya kuripoti kazini.
Pia Makamu wa Rais amesema Chuo cha Utumishi wa Umma kinapaswa kujipanga kutoa elimu itakayowajengea wahitimu uwezo wa kujiajiri na kuwa na ubunifu ambao utawasaidia kuchangamkia fursa zinazojitokeza.
Amesema
ni muhimu Chuo hicho kuhakikisha wakati wote kinatoa elimu inayoendana na mahitaji ya soko na mabadiliko ya teknolojia inayokua kwa kasi pamoja na vipaumbele vya kitaifa ikiwamo ujenzi wa uchumi wa viwanda, uchumi wa buluu, uchumi wa kidigiti, nishati jadidifu, na kukabiliana na athari za
mabadiliko ya tabianchi.
Makamu wa Rais amesema Serikali imejipanga kuhakikisha sekta ya elimu inaboreshwa zaidi ili kukidhi mahitaji na kuendana na jitihada za kuleta maendeleo endelevu nchini. Ameongeza kwamba Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya Vyuo na kuongeza udahili ili wananchi zaidi wapate
fursa ya kujiendeleza kimasomo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene wakati alipowasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es salaam kushiriki Mahafali ya 39 ya Chuo Cha Utumishi wa Umma Tanzania tarehe 06 Juni 2024.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...