*TAKUKURU Kuendelea kutoa elimu ili kuwaepusha watanzania na mkono wa sheria

Na Leandra Gabriel, Dar es Salaam

TAASISI Ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU,) imeeleza kuwa inatambua mchango dini katika kutoa maadili sahihi kwa waumini na kuelimisha juu ya vitendo vya rushwa pamoja na kutoa maonyo kwa waumini, wagombea na wafuasi kujiepusha na vitendo vya rushwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu na uchaguzi mkuu wa 2025.

Akizungumza katika Ofisi za TAKUKURU Mkoa wa Ilala leo jijini Dar es Salaam Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Bi. Neema Mwakalyelye amesema; Kikatiba Serikali haina dini ila inatambua wananchi wana dini na vitabu vyote vya dini vina makatazo na kuitambua rushwa kama tendo ovu.

"Katika mapambano dhidi ya rushwa Taasisi pekee haiwezi kufikia Umma wa Watanzania wote na tunatambua nguvu na mchango wenu katika kujenga uadilifu kwa watanzania kupitia mafundisho na mihadhara, Tunaamini kupitia kwenu watanzania watafahamu zaidi athari za rushwa na kuepukana nayo kwa kutoa au kupokea." Amesema.

Amesema, Viongozi wa dini wana ushawishi mkubwa kwa waumini wao na kupitia kikao hicho watapata fursa ya kueleza vitendo vinavyoashiria rushwa katika uchaguzi pamoja na kukumbushana juu ya nafasi yao kama viongozi wa dini na kutoka na mikakati katika kuchangia upatikanaji wa haki nchini kwa kuwa rushwa ni adui wa haki.

Kuhusiana na vitendo vya rushwa katika chaguzi zilizopita Bi. Neema amesema kuwa vitendo vya rushwa vilikuwepo walipokea taarifa na kuchukua hatua na kutaja vitendo vya rushwa vilivyoripotiwa ni pamoja na baadhi ya wagombea kutoa Fedha, vitu, na chakula huku mkakati wao ukiwa kufika eneo la tukio na kuchukua hatua na zaidi ni kutoa elimu kwa Umma kuhusu viashiria vya rushwa pamoja na kuacha vitendo vya rushwa kwa kutopokea au kuomba rushwa kwa wagombea.

"Tumelenga sana kuwaepusha watanzania wasiingie katika vitendo vya rushwa ili wasijikute katika mgogoro wa kisheria na TAKUKURU kwa sababu lengo letu ni kuona uchaguzi unakuwa huru na haki na viongozi wanachaguliwa kutokana na uwezo wao wa kuongoza na sio rasilimali walizonazo kwa kuwa tunahitaji viongozi waadilifu na wazalendo mustakabali wa maendeleo ya Taifa." Amesema.

Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT,) Dkt. Alex Malasusa amesema kikao kazi kilichowakutanisha viongozi wa dini na TAKUKURU kimelenga kukumbushana wajibu wao katika kuzuia, kupinga na kufundisha athari za rushwa.

" Ombi kwa watanzania wenzangu tukatae rushwa na tumepewa Mamlaka na TAKUKURU ya kutoa taarifa ya nani kapokea au katoa rushwa ili tupate viongozi ambao Mungu amewatayarisha na sio fedha au jambo lolote limewatayarisha kuwa katika uongozi....Kama mjuavyo katika misaafu yote inakataza kula rushwa na sisi kama viongozi wa dini tunaishukuru sana Taasisi hii kwa kutukusanya pamoja na kukumbushana kuhusu jambo hili." Amesema.

Aidha ameeleza kuwa, majadiliano hayo yamelenga katika kujadili udhibiti wa vitendo vya rushwa katika kuelekea uchaguzi, kabla, baada na wakati wa uchaguzi kwa kuwa rushwa ni adui wa haki na katika biblia imeeleza kuwa rushwa hupofusha.

"Baada ya rushwa mtu hawezi kuona malengo ya kulitumikia Taifa aliyotumwa, Tumefurahi kupata fursa hii na tutaendelea kuwahimiza watanzania kukataa kutoa na kupokea rushwa kwa vitendo katika maisha yetu yote na kuelekea uchaguzi tusiwe na mawazo ya kutoa au kupokea rushwa ili kutendea haki nafasi zetu za kuchagua na kuchaguliwa." Amesema.

Pia Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania Sheikh. Dkt. Alhad Juma Salum ameishukuru TAKUKURU kwa kuona nafasi ya viongozi wa dini katika suala hilo na kutoa mchango wao katika kupambana na rushwa hususani katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

"Kwa niaba ya viongozi wa dini zote tunaishukuru sana TAKUKURU na hii inaonesha dhamira njema ya Taasisi hii ya kutaka kuona kwamba uchaguzi huu hautawaliwi na rushwa na ni jambo jema sana kwa mustakabali wa Taifa kwa ujumla." Ameeleza.

Ameeleza kuwa, Viongozi wa dini wapo pamoja katika kufikisha ajenda hiyo kwa wananchi ili kushirikiana katika kupambana na kuziba mianya ya rushwa na kuhakikisha haina nafasi katika jamii kwa kuwapa mafundisho ya kidini na hofu ya Mungu.

Pia kiongozi wa Kanisa la Inuka Uangazee; Nabii na Mtume Boniface Mwamposa amesema kuwa, TAKUKURU imeona umuhimu wa viongozi wa dini katika kujadili suala la udhibiti wa vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi na kuwakusanya kwa majadiliano ya jinsi ya kusaidia Taifa dhidi ya vitendo hivyo ili Taifa lipate viongozi wenye kuzingatia haki, usawa na uzalendo.

" Sisi kama viongozi wa dini tutatumia neema na madhabahu katika kuwasaidia watu kufahamu hatari ya rushwa na baraka ya kukataa rushwa na tunatoa mwito kwa watanzania kabla ya sheria kuanza kufanya kazi neema ya Mungu imsaidie mtu kujua siri ya baraka.....Ukianza maisha ya kuchukua au kula rushwa moja kwa moja unaingia kwenye laana ila ukianza kusimama katika haki unasimama kwenye baraka." Ameeleza Mwamposa.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU,) Bi. Neema Mwakalyelye akifungua kikao hicho kilichowakutanisha na viongozi wa dini na kueleza kuwa TAKUKURU inatambua mchango dini katika kutoa maadili sahihi kwa waumini na kuelimisha juu ya vitendo vya rushwa pamoja na kutoa maonyo kwa waumini, wagombea na wafuasi kujiepusha na vitendo vya rushwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT,) Dkt. Alex Malasusa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kikao kazi kilichowakutanisha viongozi wa dini na TAKUKURU na kueleza kuwa kimelenga kukumbushana wajibu wao katika kuzuia, kupinga na kufundisha athari za rushwa. Leo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania Sheikh. Dkt. Alhad Juma Salum akizungumza kuhusiana na mkutano huo ambapo ameishukuru TAKUKURU kwa kuona nafasi ya viongozi wa dini katika suala hilo na kutoa mchango wao katika kupambana na rushwa hususani katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
kiongozi wa Kanisa la Inuka Uangaze;  Nabii na Mtume Boniface Mwamposa akizungumza kuhusiana na kikao kuwa, TAKUKURU imeona umuhimu wa viongozi wa dini katika kujadili suala la udhibiti wa vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi na kuwakusanya kwa majadiliano ya jinsi ya kusaidia Taifa dhidi ya vitendo hivyo ili Taifa lipate viongozi wenye kuzingatia haki, usawa na uzalendo.




 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...