MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA,) imewashauri watendaji wa soko hilo zikiwemo kampuni na taasisi zinazopewa leseni na CMSA pamoja na wadau wa sekta ya masoko ya mitaji ambao wangependa kufanya kazi na CMSA kutumia fursa ya mafunzo maalumu ya kitaaluma yatakayotolewa na mamlaka hiyo.

Lengo la mafunzo hayo ni kupata weledi wenye tija na viwango vya kimataifa ambayo pia yatawasaidia washiriki kufanya kazi katika masoko yaliyo nje ya mipaka.

Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya maonesho ya Biashara maarufu kama Sabasaba jijini Dar es Salaam, Ofisa Uhusiano na Elimu kwa Umma Stella Anastas kutoka CMSA amesema katika msimu huu wa Sabasaba mamlaka hiyo imekuja na programu ya elimu ya mpango wa mafunzo endelevu ya Kitaaluma.

Ambapo amesema Mamlaka hiyo imeianzisha na itaanza mwaka huu wa fedha na kwamba mpango huo ni moja kati ya mkakati wa utekelezaji wa elimu jumuishi ya fedha ambao pia unalenga kutekeleza mpango mkuu wa sekta ya fedha.

"Chini ya mpango huu wataalam wa soko nikimaanisha kampuni na taasisi mbalimbali ambazo utendaji wake unategemea kupata leseni kutoka CMSA wanatakiwa kuwa na jumla ya saa 35 kwa mwaka chini ya programu hii.

"Saa hizo zimegawanyika katika makundi mawili ambapo kundi la kwanza la structured program ambayo itawataka watendaji kushiriki katika programu mbalimbali zilizoandaliwa kwa saa 21 na saa 14 yatatokana na utendaji kazi wao wa kila siku unaolenga katika masuala ya masoko ya mitaji," amesema.

Aidha amesema katika kuhakikisha utekelezaji huo unakuwa wenye tija kwa Mamlaka, CMSA imeweka mpango huo kama moja ya maazimio makubwa katika mpango mkakati wa miaka mitano 2023/2024 na 2024/2027.

Akieleza faida kwa washiriki katika programu hiyo Stellah amesema ni pamoja na kupata fursa ya kupata maarifa pamoja na masoko yaliyopo nje ya nchi kwa kukutana na watendaji wengine wa masoko waliopo nje ya nchi na namna wanavyotekeleza majukumu yao na wanavyopambana na changamoto katika masoko na kutumia weledi huo kuleta tija katika masoko ya nchini.

Ameongeza kwamba programu hiyo itawasaidia katika kuwalinda wateja na wawekezaji wa masoko ya mitaji wanaotumia huduma zao kutokana na weledi zaidi kupitia mafunzo.







 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...