Taasisi ya kimataifa ya Nos Vies en Partage (NVeP), kwa kushirikiana na kampuni ya Barrick, imetoa msaada wa dola za Kimarekani 20,000 kwa  shule mbili za sekondari za Kilakala iliyopo mkoani Morogoro na  Victory iliyopo mkoani Arusha kila moja dola 10,000 kwa ajili ya kuendeleza miradi ya kukuza taaluma kutokana na kufanya vizuri katika ubunifu na utekelezaji wa miradi hiyo.

Msaada huo umetokana na sehemu ya fedha zilizotolewa na taasisi ya Nos Vies en Partage (NVeP), iliyoanzishwa na inayofadhiliwa na Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Barrick Gold Corporation, Mark Bristow, kwa ajili ya kusaidia makundi maalum kama vile Wanawake, watoto na makundi mengine yenye uhitaji yasiofaidika na ukuaji wa kiuchumi barani Afrika.

 Kila robo ya mwaka taasisi ya NVeP,  imeweza kutoa misaada yenye tija na manufaa ya moja kwa moja kwenye jamii mbalimbali zenye uhitaji barani Afrika na kufikia sasa zaidi ya mashirika 20 yasiyo ya Kiserikali na taasisi za kijamii nchini yamepatiwa msaada huo na tayari umeleta mabadiliko chanya katika jamii hususani katika sekta ya elimu, afya kwa Wanawake na watoto na utunzaji wa Mazingira.

Akiongea wakati wa hafla ya kukabidhi msaada huo  jijini Dar es  Salaam , Meneja wa Barrick nchini,Melkiory Ngido, alizipongeza shule hizo kwa kufanikiwa kupata msaada huu wakati wa awamu hii na kusema kuwa taasisi ya NVeP, itaendelea kusaidia mashirika yasiyo ya kiserikali  na taasisi ambazo zinatoa huduma kwa jamii kwendana na malengo ya taasisi hiyo sambamba na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

 “Tunajivunia kuona fedha zinazotolewa na Barrick kwa kushirikiana na NVeP zinasaidia kuleta mabadiliko chanya katika jamii kwenye maeneo mbalimbali nchini na tunaamini wanufaika wa msaada huu leo  mtatumia fedha hizi kwa lengo lililokusudiwa” ,alisema Ngido.

Akiongea baada ya kupokea hundi ya fedha za msaada huo, Mkuu wa shule ya sekodari ya Kilakala ya mkoani Morogoro ,Mary Lugina  , ameshukuru Barrick kwa msaada huo na kueleza kuwa utasaidia kuboresha miradi ya kuinua taaluma shuleni hapo na kupandisha ufaulu wa wanafunzi ili waweze kukabili changamoto mbalimbali kwa kutumia elimu bora wanayoipata.

 Naye Mwakilishi wa shule ya  sekondari ya Arusha Victory, Ruth Muruve  ambaye alipokea hundi kwa niaba ya shule hiyo , ameshukuru kupatiwa msaada huo na amesema kuwa utasaidia kufanikisha programu za kuinua taaluma kwa wanafunzi wanaosoma shuleni hapo hususani  wanatoka kwenye mazingira magumu ya kifamilia.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...