Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
TUME ya Utumishi wa Mahakama imewataka wananchi wenye malalamiko mbalimbali kuhusu vitendo vya ukiukwaji wa maadili ikiwemo kuombwa rushwa unaofanywa na mahakimu na majaji wawasilishe kwa njia ya maandishi.

Imeelezwa baada ya Tume kupokea malalamiko hayo hufanya uchunguzi kujiridhisha na tuhuma zinazotolewa dhidi ya watumishi hao na ikibainika kuchukua hatua za kinidhamu.

Stephen Sumari, Ofisa wa Tume ya Utumishi wa mahakama, amesema hayo leo Julai 5,2024 jijini Dar es Salaam, katika maonesho ya sabasaba yanayoendelea ambapo amesema kuwa maadili ya msingi kwa mahakimu na majaji ni uadilifu, uwazi, usiri, uwajibikaji, ushirikiano na weledi.

Amesema endapo mahakimu na majaji wakikiuka taratibu basi wanafikishwa kwenye kamati za maadili na wakibainika kutenda makosa, wanasimamishwa kazi, kuhamishwa vituo na hata kustaafishwa kwa maslahi ya umma.

"Mwananchi mwenye malalamiko kuhusu kuahirishwa kwa kesi mara kwa mara bila sababu ya msingi, kuombwa rushwa au hata ulevi, atume malalamiko yake kwa njia ya maandishi akiambatanisha na ushahidi hii itasaidia kufanyika kwa uchunguzi wa kina na kamati itatoa maamuzi kama mtuhumiwa ana kosa au la," amesema Sumari.

Ameongeza kuwa wananchi wengi wamekuwa wakilalamika bila kupeleka malalamiko yao kwa njia ya maandishi hivyo, husababisha kukosa haki zao za msingi.

Sumari alisema malalamiko hayo yanapokelewa kwenye kamati za maadili wilaya, mkoa na kupitia kamati ya maadili ya majaji.

"Hakimu au jaji hapaswi kuchukua rushwa hivyo ukiombwa rushwa kuhusu kesi fulani utapaswa kuandika barua ikieleza taarifa za msingi kama vile namba ya kesi, unayemlalamikia anaitwa nani na kesi yako imefikia hatua gani," alifafanua.

"Tunatunza siri kwa mtu atakayewasilisha malalamiko ili asijulikane na mlalamikiwa..., Tunao wajibu wa kuziimarisha kamati za maadili ili kuimarisha maadili ya maofisa wa mahakama," amesema.

Sumari ameongeza kusema kuwa, changamoto inayowakabili ni pamoja na uelewa mdogo wa wananchi katika kufahamu majukumu ya tume pamoja na kamati zake hivyo, hawajui sehemu sahihi ya kuwasilisha malalamiko yao.

"Kwa kuwa watu wengi hawaelewi kazi ya tume, tumeandaa mpango kazi kwa ajili ya kuwasaidia makatibu tarafa wa vijiji na kata kufanya kazi ya kuitangaza tume kwa wananchi.

Tume hiyo mwenyekiti wake ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Profesa Ibrahimu Juma, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi na wajumbe wawili wanaoteuliwa na Rais.

Moja ya majukumu yao ni kusimamia ajira na nidhamu za watumishi wa mahakama kwa mujibu wa Ibara ya 113(1) ikisomwa pamoja na kifungu namba 29(1) cha Sheria ya Usimamizi Mahakama namba 4 ya mwaka 2011.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Ibrahimu Juma akipata maelekezo kutoka kwa Ofisa wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Stephen Sumari wakati alipotembelea banda la Tume hiyo leo Julai 5,2024 katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...