Mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu ya NBC, Benki ya NBC imesema mpango mpya wa utoaji wa tuzo kwa wachezaji bora wa kila mechi za ligi hiyo ni mwendelezo tu wa jitihada za benki hiyo katika kunogesha ligi huku ikibainisha kuwa bado kuna mipango mizuri zaidi inaandaliwa ikilenga kuongeza mvuto, ushindani na vinwango kwenye ligi hiyo.
Kauli ya mdhamini huyo anaedhamini ligi tatu muhimu za mpira wa miguu hapa nchini imekuja huku tayari ikishuhudiwa wachezaji kutoka vilabu mbalimbali vinavyoshiriki ligi Kuu ya NBC, wakipatiwa tuzo za uchezaji bora kwenye mechi nne ambazo zimekwisha chezwa kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo.
Alikuwa Mlinda mlango wa timu ya Pamba Jiji ya jijini Mwanza, Yona Amosi Abel ndio aliefungua pazia la kutwaa tuzo hizo baada ya kuibuka mchezaji bora kwenye mechi ya kufungua pazia la ligi hiyo baina ya timu hiyo na Prisons ya mkoani Mbeya, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na kuisha kwa suluhu ya bila kufungana.
Maofisa wa benki ya NBC Tawi la Mwanza wakiongozwa na Meneja wa Benki hiyo tawi la Nyanza jijini humo Innocent Ngavatula ndio pia walifungua pazia la kukabidhi zawadi hizo wakifuatiwa na maofisa wengine wa benki hiyo katika mikoa tofauti zilipochezwa mechi za ligi hiyo ikiwemo Kigoma, Mbeya na Dar es Salaam.
“Tukiwa tumetambulisha rasmi tuzo hizi kwenye kila mechi ya ligi hii, tayari tumekabidhi jumla ya tuzo nne kwa wachezaji wa vilabu tofauti ambavyo tayari vimecheza michezo yao. Mbali na Yona Amosi wa Pamba jiji tuzo hizi pia tumekabidhi kwa Mlinzi wa kati wa klabu ya Mashujaa FC Ibrahim Ame, Kiungo Emmanuel Keyekeh ‘The Sniper’ kutoka Singida Black Stars na Beki wa Simba SC, Che Fondoh Malone’’ alitaja David Raymond, Mkuu wa Idara ya Masoko benki ya NBC.
Kwa mujibu wa Raymond, ujio wa tuzo hizo za wachezaji bora kila mechi haujaathiri kwa namna yoyote utaratibu wa wa awali wa kutoa tuzo za mchezaji na kocha bora wa ligi hiyo kila mwezi.
“Lengo haswa ni kuhakikisha ndani ya muda mfupi tunakuwa na vionjo vingi zaidi kwenye ligi hii tukilenga kuongeza chachu na ushindani kwenye ligi husika kupitia utambuzi wa jitihada zinazofanywa na wachezaji wetu na mabenchi yao ya ufundi katika ubora.’’
‘’Kupitia ushirikiano wetu na Shirikisho la mpira wa Miguu nchini (TFF) pamoja na wadau wengine wakiwemo wataalam mbalimbali wa mchezo huu tutaendelea kubuni mambo mazuri yenye tija zaidi kwa faida ya wadau wote wa ligi hii wakiwemo pia mashabiki’’ alibainisha.
Ikiwa kama mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu ya NBC, Ligi ya Championship na Ligi ya Vijana, benki ya NBC imekuwa ikitoa huduma mbalimbali za kibenki zinazolenga kuvisaidia vilabu vinavyoshiriki ligi hiyo ikiwemo utoaji wa mikopo ya mabasi kwa baadhi ya vilabu na bima za afya kwa wachezaji na mabenchi ya ufundi.
“Zaidi tumekuwa tukishiriki katika kuandaa sherehe za ubingwa kwa washindi wa ligi zote tunazozidhamini pamoja na kudhamini matukio mbalimbali ya kimichezo yanayoandaliwa na TFF na wadau wengine wa michezo hapa nchini ikiwemo serikali,’’ alisema.
Mkuu wa Kitengo cha Biashara Benki ya NBC, Ibrahimu Nzutu (Kulia) akikabidhi tuzo kwa Beki wa timu ya Simba SC, Che Fondoh Malone aliyetangazwa mchezaji bora kwenye mechi ya Ligi Kuu ya NBC mzunguko wa kwanza baina ya timu hiyo na timu Tabora United ya mkoani Tabora. Makabidhiano hayo yalifanyika baada ya kukamilika kwa mchezo baina ya timu hizo mbili uliofanyika katika Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Mchezo huo uliiisha kwa timu ya Simba SC kuibuka na ushindi wa 3-0. Benki ya NBC ni mdhamini mkuu wa ligi hiyo.
Meneja wa Benki ya NBC tawi la Nyanza jijini Mwanza Innocent Ngavatula (wa tatu kushoto) akikabidhi tuzo kwa Mlinda mlango wa timu ya Pamba Jiji ya jijini Mwanza, Yona Amosi Abel (wa tatu kulia) aliyetangazwa mchezaji bora kwenye mechi ya Ligi Kuu ya NBC mzunguko wa kwanza baina ya timu hiyo na timu ya Prisons ya jijini Mbeya. Makabidhiano hayo yalifanyika baada ya kukamilika kwa mchezo baina ya timu hizo mbili uliofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza mwishoni mwa wiki. Mchezo huo uliiisha kwa suluhu ya bila kufungana. Wengine ni maofisa wa benki ya NBC mdhamini mkuu wa ligi hiyo.
Meneja wa Benki ya NBC tawi la Kigoma, Athuman Fumbuka (kulia) akikabidhi tuzo kwa Mlinzi wa kati wa klabu ya Mashujaa FC, Ibrahim Ame aliyetangazwa mchezaji bora kwenye mechi ya Ligi Kuu ya NBC mzunguko wa kwanza baina ya timu hiyo na timu ya Dodoma Jiji ya jijini Dodoma. Makabidhiano hayo yalifanyika baada ya kukamilika kwa mchezo baina ya timu hizo mbili uliofanyika katika Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma mwishoni mwa wiki. Mchezo huo uliiisha kwa timu ya Mashujaa FC kuibuka na ushindi wa goli 1-0. Benki ya NBC ni mdhamini mkuu wa ligi hiyo.
Meneja Huduma na Uendeshaji Benki ya NBC tawi la Mbeya Stanslaus Sana (kulia) akikabidhi tuzo kwa Kiungo Emmanuel Keyekeh ‘The Sniper’ kutoka Singida Black Stars aliyetangazwa mchezaji bora kwenye mechi ya Ligi Kuu ya NBC mzunguko wa kwanza baina ya timu hiyo na timu ya KenGold FC ya jijini Mbeya. Makabidhiano hayo yalifanyika baada ya kukamilika kwa mchezo baina ya timu hizo mbili uliofanyika katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya mwishoni mwa wiki. Mchezo huo uliiisha kwa timu ya Singida Black Stars kuibuka na ushindi wa goli 3-1. Benki ya NBC ni mdhamini mkuu wa ligi hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...