Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuelekeza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Charles Msonde kuhakikisha anazisimamia Taasisi za Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kufanya mabadiliko na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazokabili Taasisi hizo ili kuboresha utendaji na ufanisi wa Taasisi hizo.
“Namjua Dkt. Msonde nimefanya nae kazi nikiwa TAMISEMI, ni mzee wa kunyooka na mwenye kufuata utaratibu, kwa hiyo naomba mnipe miezi mitatu nimkabidhi Taasisi hizi Naibu Katibu Mkuu ili kufanya mabadiliko katika taasisi hizi”, amesema Bashungwa.
Ametoa maelekezo hayo Agosti 20, 2024 jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya ukarabati na ujenzi wa vivuko vipya kutoka kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu jijini Dodoma na kuahidi Kamati hiyo kumpa miezi mitatu ili kufanya mabadiliko kwa Taasisi hizo.
Waziri Bashungwa ameeleza kuwa Dkt. Msonde atamsaidia Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kufanya maboresho katika Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo.
Aidha, Bashungwa ametumia fursa hiyo kumshukuru Mhe. Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa uteuzi wa Niabu Katibu Mkuu huyo pamoja na kumpongeza Naibu Katibu Mkuu aliyepita Bw. Ludovick Nduhiye ambaye kwa sasa ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi kwa utendaji mzuri wakati akiwa Wizara ya Ujenzi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Selemani Kakoso amesisitiza umuhimu wa Wizara ya Ujenzi kusimamia TEMESA na TBA ziweze kukusanya madeni wanayodai kwa Taasisi za Serikali ili kuisaidia Wakala hizo kujiendesha pamoja na kutoa gawio kwa Serikali.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...