Na WILLIUM PAUL, Siha.

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga amewataka Viongozi wa Kata na Wahudumu wa afya ngazi ya jamii kushirikiana kuwatambua wagonjwa waliofichwa ndani na watu wenye ulemavu ili waweze kupata haki yao ya msingi ya kupata huduma ya afya hatimaye kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Nderiananga alitoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo viongozi wa Kata na wahudumu wa afya ngazi ya jamii 170 yaliyoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Apotheker Health Access Initiative kwa kushirikiana na Taasisi ya Dkt. Godwin Mollel Mbunge wa Jimbo la siha na Naibu Waziri wa Afya.

Alisema kuwa, kila mwananchi ana haki ya kupata matibabu sahihi kwa mujibu wa sheria bila kujali hali yake ikiwa ni mwenye ulemavu au hana ulemavu huku akiwasisitiza kuwa sehemu ya faraja kwa wagonnjwa badala ya kuwanyanyapaa.

Aliwahimiza kufanya kazi kwa ushirikiano hatua itakayosaidia kuwafichuwa baadhi ya wagonjwa waliofichwa ndani na kukosa matibabu pamoja na kuisaidia jamii kwa kutoa elimu ya masuala ya afya kwa lengo la kuepukana na magonjwa mbalimbali hatimaye kuwa na jamii yenye afya bora.

“Viongozi wa Kata na wahudumu wa afya ngazi ya jamii nyinyi mna jukumu kubwa sana la kuhakikisha mnavumbua wagonjwa waliofichwa, aidha wagonjwa au wenye ulemavu kwani na wao wana haki ya kupata huduma, tusiwaweke ndani watoeni ili wapate msaada kwa sababu kumfungia ndani kunahatarisha afya yake na utakuwa umemfanyia ukatili,” Alisema Mhe. Nderiananga.

Naye Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel alieleza kwamba ni muhimu kwa viongozi wa Kata na wahudumu wa afya ngazi ya jamii kushirikiana katika kuhakikisha usalama wa afya za wananchi katika maeneo yao zinaimarika kwani wao ni watu wa karibu zaidi na jamii husika.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...