Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amemwagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ama Naibu Waziri wake, kuungana nae ziarani Kagera kwa ajili ya kuyatolea ufafanuzi malalamiko ya wananchi yanayohusu upatikanaji wa Vitambulisho vya Uraia (almaarufu NIDA).
Balozi Nchimbi ambaye yuko katika ziara yake ya siku 6 mkoani Kagera, ametolea maelekezo hayo aliposimama kuwasalimia wananchi wa Kyerwa, katika Uwanja wa Nkwenda Maziwa, akiwa njiani kuelekea Karagwe, leo Alhamis Agosti 8, 2024.
“Tangu nimeanza ziara maeneo ya Mkoa wa Kigoma na hapa Mkoa wa Kagera wananchi wanalalamikia upatikanaji wa Vitambulisho vya NIDA. Hapa pia ninyi kupitia kwa Mbunge wenu Innocent Bilakwate mmelilalamikia.
“Nimeshatolea maagizo mahali pengine mchakato wa upatikanaji wa vitambulisho vya NIDA uboreshwe na uharakishwe ili wananchi wapate utambulisho wao. Na nimesema wananchi kudai vitambulisho ni dalili ya mapenzi kwa nchi yao.
“Lakini kupitia mkutano huu, naomba kumwelekeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi au Naibu Waziri wake, aungane nasi awe sehemu ya msafara wa ziara yangu ili atolee ufafanuzi malalamiko ya wananchi kuhusu Vitambulisho vya Uraia,” amesema Balozi Nchimbi.
Katika ziara hiyo, yenye malengo ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, kuhamasisha uhai wa chama na kuwasikiliza wananchi, Katibu Mkuu wa CCM Balozi Nchimbi ameambatana na Ndugu Issa Haji Usi Gavu, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) - Oganaizesheni, Ndugu Amos Gabriel Makalla, Katibu wa NEC - Itikadi, Uenezi na Mafunzo na Ndugu Rabia Hamid Abdalla, Katibu wa NEC - Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, ambapo leo atakuwa Wilaya za Kyerwa na Karagwe.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...